WANANCHI wa kijiji cha Naadare, kata ya Kitumbeine, wilayani Longido
mkoani Arusha, wametoa rai kwa wasambazaji wa mbegu kwa ajili ya kilimo
wazisambaze haraka na kwa wakati ili wawahi kupanda.
Aidha, wametoa rai kwa serikali kuangalia uwezekano wa kujengwa shule
karibu na maeneo wanayoishi ili kuepuka wanafunzi kutembea zaidi ya saa
nne kwenda kupata elimu na kurudi nyumbani usiku.
Rai hiyo ilitolewa na wananchi hao jana wakati wa mkutano wa hadhara
pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo anayetembelea wilaya hiyo
na kujua kero mbalimbali zinazowakabili.
Mmoja kati ya wananchi hao, Elihuruma ole Sapuk alisema hivi sasa
wananchi wa maeneo hayo wanakosa mbegu kwa wakati na kusababisha
kushindwa kupanda kwa wakati na hivyo kuvuna mavuno kidogo.
Mwanafunzi, Elisupak ole Sapuk anayesoma shule ya msingi Lorienito
alisema, ili afike shuleni mapema analazimika kutoka nyumbani saa 11:00
alfajiri na kufika shuleni saa 4:00 asubuhi, akiwa amechoka kutokana na
kutembea umbali mrefu.
Alisema na akitoa nyumbani alfajiri anakuwa hajala chakula hivyo ni
vyema sasa wazazi na walezi kuchangia elimu ili wanafunzi waweze kusoma
kwenye maeneo yaliyo karibu na nyumbani kwao.
Mwananchi Elizabeth Senate alisema, wameamua kukusanya nguvu zao kwa
ajili ya ujenzi wa madarasa matatu eneo hilo, lakini wameshindwa jinsi
ya kupaua na kuweka huduma nyingine muhimu ili kupunguza umbali mrefu
watoto wao wanaotumia kutafuta elimu.
Gambo alisema amesikia kero ya elimu kwa watoto hao na kuahidi
kutafuta mabati na mahitaji mengine kumaliza kupaua jengo hilo la shule.
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo alisisitiza Wakala wa
Mbegu kusambaza mbegu kwa wakati kwa wananchi hao ili walime na kupata
mazao mengi yatakayowasaidia kukabiliana na ukosefu wa chakula. CHANZO:HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment