Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi
la Polisi mkoani hapa kupitia kitengo chake cha Dawati la Jinsia na
Watoto limeanza kutembelea shule za Msingi kwa nia ya kutoa elimu ya
Ukatili dhidi ya watoto. Hayo yameelezwa na Mkuu wa kitengo hicho
Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu wakati alipokuwa anatoa elimu kwa
wanafunzi wa shule ya Msingi Sombetini iliyopo halmashauri ya jiji la
Arusha.
Alisema
kwa muda mrefu wamekuwa wakipokea malalamiko mbalimbali ya wanawake,
wanaume na watoto wakiwa ofisini lakini wamegundua kwamba wanafunzi
wengi wa shule za Msingi hawana uelewa juu ya vitendo vya Ukatili
unaotokea miongoni mwao.
Akitoa
elimu hiyo kwa wanafunzi hao Mkuu huyo wa Dawati alisema kwamba baadhi
ya watoto wanafanyiwa vitendo vya ukatili kwa kubakwa na kulawitiwa
lakini ukaa kimya na wasijue nani wa kumwambia, hivyo kuwataka pindi
wanapoona dalili za watu kutaka kuwafanyia vitendo vya aina hii watoe
taarifa haraka kwa wazazi wao, majirani au walimu.
Alisema
kumekuwa na mbinu tofauti tofauti zinazotumiwa na walaghai kama vile
kumnunulia Mwanafunzi pipi, kumpa msaada wa kumpeleka shule na
kumrudisha nyumbani “lift”, kumpa pesa hali ambayo aliwaambia wanafunzi
waikatae kwani sio watu wote wana nia nzuri na wao.
“Mara
unapohisi kuna mtu ambaye anasogea karibu yako na kukudanganya kwa
kukupa msaada wa lift au kukunulia pipi unatakiwa kutoa taarifa mapema
kwa wazazi wako, walezi wako, majirani au walimu wako hali ambayo
itasaidia kukuepusha kuingia kwenye matatizo”. Alisisitiza Mkuu huyo wa
Dawati.
Alisema
watoto wanaweza wakafanyiwa vitendo hivyo si kwa watu wa nje na nyumba
zao tu bali hata watu wao wa karibu kwa maana ya wazazi au walezi wao
wanaweza kuwafanyia vitendo hivyo, na kuwaeleza kwamba wana nafasi ya
kuwaeleza majirani na walimu wao ambapo taarifa hizo baadae zitawafikia
katika ofisi yao ya Dawati na wao kuchukua hatua mara moja.
Akizungumzia
aina mbalimbali za ukatili askari wa kitengo hicho, Happy Mshana
alisema kwamba ukatili upo wa aina tofauti tofauti kama vile ukatili wa
kingono, ukatili wa kijinsia, ukatili wa Kisaikolojia, ukatili wa
kielimu na kadhalika.
Alisema
mara nyingi wanafunzi wanaathirika na ukatili wa kielimu ambapo hali
hii inatokana na wazazi au walezi kuwazuia watoto wao kwenda shule huku
wakiwa wanastahili kusoma, hivyo kuwataka pindi wanapoona wao au wenzao
wanakumbwa na hali hii watoe taarifa kwa majirani na ikishindikana
wawaeleze walimu wao.
Kutokana
na elimu iliyotolewa na Dawati hilo iliweza kuibua hisia za wanafunzi
mbalimbali ambao wengi waliuliza maswali ambayo yalijibiwa na askari wa
kitengo hicho walioongozwa vyema na Mkuu wa kitengo hicho Mkaguzi wa
Polisi Happyness Temu, huku wengi wao wakionekana kushangilia baada ya
mmoja wao kutaka adhabu ya kunyongwa itumike kwa watuhumiwa wanaokutwa
na hatia kwa makosa ya ubakaji na ulawiti badala ya kifungo.
Mwanafunzi wa darasa la sita aitwaye Jackson Mutalemwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Haki za Watoto
(Children Right Club) alisema kwamba kitendo cha Dawati kutoa elimu
shuleni hapo kimekuja muda muafaka kutokana na vitendo hivyo kuripotiwa
kwenye Klabu yao mara kwa mara hasa wanavyofanyiwa watoto wa mitaani
hivyo kuwataka wasiishie kwenye shule tu bali wawaelimishe pia watoto wa
mitaani
0 comments:
Post a Comment