Home » » Serikali kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi

Serikali kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi



Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
08/09/2016
Serikali imesema imejipanga kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi inayotokana na wathamini kutozingatia maadili ya uthamini pamoja na kazi za uthamini kufanywa na watu wasiokuwa na sifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Willium Lukuvi leo mjini Dodoma alipokuwa akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini mwaka 2016 katika mkutano wa nne wa kikao cha tatu cha  Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Lukuvi amesema kuwa lengo kuu la Muswada huo ni kutunga Sheria itakayoweza kusimamia taaluma na shughuli za uthamini Tanzania Bara kwa kupunguza changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na sekta ya ardhi kwa ujumla.

Aidha, Waziri huyo amesema kuwa sheria hiyo iliyopendekezwa itasaidia katika kuwaondolea mateso wananchi wanaothaminiwa mali zao na kuchelewa kulipwa fidia kwa kuweka ukomo wa muda ambao fidia hiyo lazima ilipwe na kuwadhibiti wawekezaji kulipa fidia kwa wakati.

Pia ameongeza kuwa sharia hiyo itasaidia kuondoa utapeli uliokuwa unafanywa na wathamini  kuongeza thamani kinyume na utaratibu na kuongeza wafidiwa hewa sambamba na kuthibiti uthamini wa kifisadi ambao umekuwa ukifanywa na wathamini kwa kushusha thamani ya mali kwa madhumuni ya kukwepa kulipa kodi.

Zaidi ya hayo, katika usajili wa wathamini chini ya sheria hiyo inayopendekezwa, kutakuwa na mfumo wa kuwawajibisha wathamini ambao watakaokiuka maadili ya kitaaluma, kutoa adhabu kwa wathamini wanaokiuka sharia hiyo ikiwa ni pamoja na kifungo, faini kali na kusimamishwa au kufutiwa usajili.

Kwa upande wake Waziri Kivuli kambi ya upinzani katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Wilfred Lwakatare amesema kuwa sheria hiyo ikitekelezwa itasaidia kupunguza changamoto katika sekta ya ardhi na nyumba zilizokuwa zinatokana na matatizo ya uthamini.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa