UONGOZI wa Mkoa wa Arusha umeisimamisha kazi Bodi na Menejimenti ya
Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos) ya Kurugenzi Saccos kilicho chini ya
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa tuhuma za ufisadi na imeagizwa wahusika
kufikishwa mahakamani.
Taarifa ilitolewa jana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard
Kwitega, ilieleza kuwa bodi hiyo na menejimenti yake, imesimamishwa kazi
kutokana na tuhuma za ufisadi wa mfuko wa wanachama wa Saccos hiyo
wenye thamani ya Sh milioni 600.
Kwitega alisema amemuagiza Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika mkoa
wa Arusha, Nerei Kyara, kuchukua hatua za kisheria kwa kuwafikisha
mahakamani watuhumiwa wote.
Pia Kwitega ameagiza kuchukuliwa taratibu zinazohusiana na sheria ya
vyama vya ushirika, ikiwa ni pamoja na kuitisha mkutano mkuu maalumu wa
wanachama wa Saccos hiyo.
Alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya idadi kubwa ya wanachama
kulalamika kutokupewa mikopo pia mikopo kutolewa kinyume cha taratibu
kwa taasisi binafsi, tofauti na utaratibu wa Saccos unavyoelekeza.
Aliwataja waliosimamishwa kuwa ni Mwenyekiti wa Bodi, Dk Freedom
Makiago kutoka Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na wakurugenzi wa bodi
hiyo, Meneja wa Saccos hiyo, Christine Sumaye na Menejimenti.
Katibu tawala huyo alitoa muda wa siku 10 kwa Mrajisi wa Vyama vya
Ushirika mkoa wa Arusha, kuanzia juzi kuchukua hatua kumaliza mgogoro
huo.
Alisema Kurugenzi Saccos inadaiwa mamilioni ya fedha kutoka kwa
taasisi za fedha, kama vile benki ya CRDB na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi
ya Jamii (NSSF).
Hivi karibuni wanachama wa Kurugenzi Saccos kwenye mkutano mkuu
maalumu uliofanyika mwezi uliopita, walimuomba Katibu Tawala wa Mkoa
kusitisha makato ya mishahara yao kulipia mikopo kwenye chama hicho kwa
kuwa hawakuelewa hatima ya fedha zao.
Wanachama hao wakiwemo wastaafu wa Hospitali ya Mount Meru, walisema
kwa kipindi kirefu Bodi ya Mikopo ya Saccos hiyo, imeshindwa kuwakopesha
kwa kukiuka taratibu za taasisi za fedha.
HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment