WADAU wa maendeleo katika Jiji la Arusha na viunga vyake wameshauriwa
kushirikiana na kujadili mpango kabambe wa maendeleo ya mpango mji
badala ya kila mtu kuvutia upande wake.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, amewasihi madiwani wa
Halmashauri ya Jiji la Arusha, Halmashauri ya Meru kuhakikisha majengo
yote ya serikali na taasisi za umma yanapimwa ili kudhibiti wavamizi wa
ardhi.
Ntibenda aliyasema hayo jana jijini hapa wakati alipokuwa akizungumza
na madiwani wa Halmashauri zote tatu ambao baadhi yao ni wapya walikuwa
wakipewa mafunzo kwa ajili ya mpango kabambe wa Jiji la mji Arusha uwe
wa kisasa.
Alisema mpango huo umelenga kuboresha Jiji la Arusha na serikali
imetumia zaidi ya Sh bilioni nane kwa ajili ya kuhakikisha majiji ya
Arusha na Mwanza yanapangwa vizuri .
Alisema ni vyema madiwani hao ambao baadhi yao ni wapya kuhakikisha
wanaojua mpango huo pamoja na kuupitisha kwenye Baraza la Madiwani ili
uweze kupitishwa na kuanza kazi Julai. Mbunge wa Arumeru Mashariki,
Joshua Nassari, aliomba madiwani wa halmashauri zote tatu kuhakikisha
wanasimamia maazimio ya Baraza la Madiwani ili kusimamia mpango huo.
Mwenyekiti wa Mipango Miji wa Jiji la Arusha, Diwani wa Moshono,
Paulo Matsei, aliwataka wanasiasa kuacha siasa badala yake wasimamie
sheria kudhibiti wanaoharibu maendeleo.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilisaini mkataba wa
makubaliano na Kampuni ya Subrana International Pty Ltd ya nchini
Singapore kwa ajili ya kuendeleza majiji ya Arusha na Mwanza pamoja na
viunga vyake.
Makubaliano hayo zilisainiwa mwaka juzi jijini Arusha na mkataba huo
wa makubaliano unatakiwa ukamilike Julai 2016 huku kazi kubwa ikiwa ni
kupanga Mji wa Arusha kuwa wa kisasa zaidi.
0 comments:
Post a Comment