Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Tume ya Uchaguzi (NEC).
Shahidi wa upande wa madai katika kesi ya kupinga
matokeo ya uchaguzi wa ubunge Jimbo la Longido, Dk. Steven Kiruswa,
ameiambia mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kuwa alikosa ubunge wa jimbo
hilo baada ya mgombea ubunge wa Chadema Onesmo Ole Nangole aliyeshinda
kuanzisha fujo chumba cha kujumlishia matokeo.
Akizungumza mjini hapa jana wakati akitoa ushahidi wake mbele ya
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Sivangilwa Mwangesi, Dk.
Kiruswa ambaye alikuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM,
alidai Nangole alipoona ameshindwa alimwaga maji mezani na kuchomoa
nyaya za kompyuta ya Tume ya Uchaguzi (NEC).
Alidai baada ya kuona hali hiyo, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Felix
Kimario, alitangaza kuahirisha kazi ya kujumlisha matokeo na yeye
aliondoka na mawakala wake kwenda nyumbani kwake, huku akiwa anaongoza
kwa kura 1,377.
"Lakini nikiwa nyumbani baada ya kukaa kwa zaidi ya dakika 15
wafuasi wangu walinishauri turudi chumba cha majumuisho na tulirudi, ila
cha kushangaza nilikuta mgombea wa Chadema (Nangole) amebebwa juu
ameshatangazwa mshindi na mimi nilipiga hesababu sikujua muujiza uliompa
ushindi," alisema.
Dk. Kiruswa alidai wakati wa vurugu zinaendelea alibahatika kupiga
picha na kurekodi tukio la kumwaga maji na kuchomoa nyaya na aliomba
mahakama ipokee kama ushahidi.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Juma Ramadhani na Wakili wa mdaiwa,
Method Kimomogolo, walipinga kupokelewa ushahidi huo kwa madai yeye sio
mtaalam wa picha na kompyuta.
Kwa upande wake, Wakili wa mdai, Dk. Lamwai Masumbuko, alipinga na
kuomba mahakama ipokee ushahidi huo kwasababu amerekodi kwa simu yake na
kupiga picha mwenyewe kwa simu hiyo na kuzisafisha, hivyo yeye ndio
muhusika.
Mahakama ilipokea vielelezo hivyo vya sauti iliyowekwa katika flashi, pamoja na picha.
Shahidi huyo aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa, jibu alilopata
baada ya kuondolewa chumba cha kujumlisha kura ni kwamba msimamizi wa
uchaguzi alikuwa kitu kimoja na Nangole ndio maana alimtangaza mshindi
wakati yeye na mawakala wake wakiwa hawapo.
"Hata nilipoangalia fomu ya majumulisho ilionyesha kuna shida,
maana wapiga kura walikuwa 57,808 ,waliojiandikisha na waliopiga kura
40,606 na kura halali 39,988 na zilizoharibika 767, lakini hapo kuna
kura 149 hazipo katika kura hizo zilizopigwa," aliendelea kudai.
Alisema kutokana na dosari hizo aliamua kufungua kesi mahakamani kupinga uchindi wa mbunge huyo ili ubatilishwe.
Kesi hiyo inaendelea kesho kwa upande wa mdai kuendelea kutoa ushahidi.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment