Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MAHAKAMA ya Rufaa wiki ijayo inaanza kusikiliza kesi za rufani 50 za
jinai na madai katika Kanda ya Arusha ikiwamo rufaa ya makamishna wawili
wa Jeshi wa Polisi wanaogombea nyumba ya serikali iliyopo Uzunguni
hapa.
Maofisa hao, Godfrey Nzowa ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na
Dawa za Kulevya katika Jeshi hilo amemshitaki mahakamani aliyekuwa
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akipinga
kuuziwa nyumba hiyo. Kamishna Kova hata hivyo amestaafu rasmi mapema
mwaka huu.
Kwa mujibu wa orodha ya kesi zitakazosikilizwa na majaji watatu wa
Mahakama ya Rufaa kwa mwezi mmoja mjini hapa, Nzowa anamlalamikia Kova
na wenzake kupinga kuuziwa nyumba hiyo aliyokuwa akiishi alipokuwa Mkuu
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) wa Mkoa wa Arusha.
Nyumba hiyo aliuziwa Kamishna Kova akiwa ameshahama mkoani Arusha na
wakati inauzwa Nzowa alikuwa akiishi katika nyumba hiyo, familia yake
akiwa RCO kabla ya kuhamishiwa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuendelea
na wadhifa huo, Kova akiwa bosi wake.
Orodha hiyo yenye jumla ya mashauri 50 inaonesha mahakama hiyo
itasikiliza rufani ya Wakili maarufu jijini Arusha, Median Mwale ambaye
amekata rufaa dhidi ya Jamhuri katika kesi yake ya kudaiwa kutakatisha
fedha chafu na kujipatia mabilioni ya fedha kwa njia ya udanganyifu
akiwa na wenzake watatu.
Rufani hiyo namba 395 ya mwaka 2013 ya Wakili Mwale dhidi ya Jamhuri
imepangwa kusikilizwa na majaji watatu, Mbarouk Salim Mbarouk, Bernard
Luanda na Semistocles Kaijage watakaosikiliza pia mashauri mengine kabla
ya kutoa uamuzi Machi 5, mwaka huu.
Orodha iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, E.Y. Mkwizu
inaonesha kesi nyingine yenye mvuto ni ile ya wafanyabiashara Philemon
Mang’ehe na Gesso Bajuta iliyodumu kwa miaka 20 sasa.
Katika kesi hiyo, Mang’ehe wa Kampuni ya Bukine anamdai fidia ya
mamilioni ya fedha Bajuta baada ya kudai kuharibiwa biashara yake ya
kusambaza vifaa vya ofisi katika Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda
(ICTR) mwaka 1996.
CHANZO : HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment