Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
CHAMA cha waendesha bodaboda Arusha (Uwapa), kimeiomba serikali
kuweka alama maalumu itakayowatofautisha wao na waendesha pikipiki
binafsi kudhibiti wahuni wanaotumia jina lao kufanya maandamano na
matukio maovu.
Kimeyasema hayo kutokana na maandamano yaliyofanyika mapema wiki hii
na kudai hakiwatambui waliofanya maandamano hayo, chama hicho hakina
taarifa kuhusu maandamano hayo. Mwenyekiti wa Uwapa, Godlight
Rugemalila, alisema ametoa taarifa polisi kutokana na maandamano hayo
kulaani kitendo hicho si sahihi.
Aliwataka waendesha bodaboda wote ikiwa wana jambo linalowakabili,
kwa kuwa uongozi upo, wafuate utaratibu badala ya kukurupuka. Rugemalila
alisema kuwepo kwa waendesha pikipiki waliosajiliwa na Uwapa ambao pia
wanakabiliwa na tatizo la kutokuwa na vituo maalum na wengine wa kawaida
ambao nao hujiingiza katika biashara, husababisha utata.
Alisema waendesha pikipiki wa kawaida wanawaharibia wanaofanya biashara halali wanaobeba abiria.
Alisema Uwapa hawajapanga maandamano na walipata taarifa kutoka kwa
watu binafsi na walishtushwa kusikia kuna maandamano hayo. Rugemalila
alisema wanaendelea kufanya utafiti kwa kushirikiana na polisi ili
kufahamu ni waliohusika kuratibu maandamano hayo.
Aliwashauri waendesha bodaboda wafuate sheria za usalama barabarani
kama zinavyoelekeza, wahakikishe wana leseni, kofia ngumu na waegeshe
pikipiki kwenye vituo vilivyosajiliwa.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, waendesha bodaboda waliosajiliwa na
wanaotambulika na Uwapa hadi sasa ni 2,950, vituo vilivyosajiliwa ni 144
na vituo bubu vinavyotarajiwa kusajiliwa karibuni ni 55.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment