
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA

Moto mkubwa umezuka mwishoni mwa wiki hii na kuunguza sehemu ya Mlima
Meru katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha. Taarifa za awali zinaonyesha
kuwa chanzo cha moto huo ni vitendo haramu vya urinaji wa asali ndani ya
msitu wa hifadhi hiyo.
Wananchi wapatao 200 kutoka vijiji jirani vya Olosinoni na Kisimiri Juu
wakishirikiana na TANAPA wamefanikiwa kuudhibiti moto huo ili usiweze
kuleta madhara makubwa kwa binadamu hususan wageni wanaotembelea hifadhi
kwa lengo la kupanda Mlima Meru.
Hadi sasa hakuna wageni waliodhurika na moto huo na tahadhari zote
zimechukuliwa ili kudhibiti madhara zaidi kwa binadamu na shughuli za
utalii ndani ya hifadhi.
Shirika la Hifadhi za Taifa linaendelea kuwatahadharisha wananchi juu ya
vitendo vya kuingia ndani ya hifadhi bila kibali kwa shughuli ambazo
zinaweza kuwa chanzo cha kuzuka kwa mioto hii ambayo husababisha
uharibifu wa mazingira pamoja na kuharibu vyanzo vya maji.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa moto huo unadhibitiwa kwa haraka, TANAPA
imeongeza nguvu kazi ya wananchi wakishirikiana na vyombo vingine vya
dola ili kuweza kuudhibiti moto huo.
Mwisho, taarifa kamili juu madhara yaliyosababishwa na moto huo
itatolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kuzima moto na umma
utaendelea kupewa taarifa ya maendeleo ya zoezi la uzimaji wa moto kila
wakati.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
21.09.2015
dg@tanzaniaparks.com


Moto unaoendelea kuwaka Mlima Meru katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Martin Loibooki akiongea na
wanakijiji wa Olosinoni wanaoshiriki zoezi la kuzima moto unaonendelea
kuwaka Mlima Meru katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha jana.
0 comments:
Post a Comment