Arusha
Home » » UCHAFU WA KIWANDA CHA NGOZI WAMCHEFUA WAZIRI

UCHAFU WA KIWANDA CHA NGOZI WAMCHEFUA WAZIRI

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene.
 
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene, amegeuka mbogo baada ya kukuta mazingira machafu katika kiwanda cha ngozi cha Sac International cha mkoani Arusha.
Kutokana na hali hiyo, Mbene ilimchukua dakika kadhaa kushuka ndani ya gari kutokana na harufu na hali ya uchafu unaotokana na mabaki ya ngozi kusambaa ovyo na ngozi kutohifadhiwa vizuri na hivyo kugeuka kuwa uchafu.

Akizungumza na watumishi wachache wa kiwanda hicho raia wa Pakistan, alisema pamoja na mazingira ya ngozi kuwa ni yenye uchafu na harufu, lakini wanapaswa kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na kupunguza harufu na uchafu.

"Uzalishaji wa ngozi unakuta harufu na uchafu kwa mazingira, lakini ni lazima mwenye kiwanda apunguze athari za uchafuzi wa mazingira, mmesambaza mabaki ya ngozi na ngozi pasipo utaratibu...hii hairidhishi kabisa, mnafanya kazi nzuri lakini hii haikubaliki," alisema Waziri Mbene.

Aidha, alisema mara kwa mara watu wa mazingira wanamfikishia malalamiko kuwa viwanda vinachafua mazingira.

Kwa mfano, kiwanda hiki ni wazi kuwa suala la utunzaji wa taka zinazozalishwa na kiwanda umewekwa kando.

Hata hivyo, alimwagiza Ofisa Biashara wa Mkoa kuhakikisha wanavitembelea viwanda hivyo mara kwa mara kwa kuhakikisha mazingira ni safi na yenye ubora na siyo kugeuka kero na yenye athari kwa Watanzania.

"Nimetembea nchi mbalimbali nimeona viwanda vya ngozi vinavyofanya kazi kukiwa na mazingira ya usafi kuanzia nje hadi ndani, huwezi kukuta hali kama hii...ngozi zimesambazwa ovyo huku mabaki ya ngozi ya kimwagwa nje na maji yakitiririka ovyo na ndani kukiwa hakujasakafiwa," alisema.

Hata hivyo, aliahidi kwamba atatembelea tena kiwanda hicho wakati mwingine ili serikali ichukue hatua mbalimbali kwani hali iliyopo siyo ya kuridhisha kwa afya za wafanyakazi na watu wengine.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa