Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amedai mshtakiwa
aliyejifanya Jaji mstaafu, Barnabas Samatta, alimtisha kuwa
angehakikisha anashindwa katika rufaa yake ya kupinga kuvuliwa ubunge.
Lema alidai kuwa baada ya kutotoa ushirikiano, mtu huyo alimtisha kuwa atahakikisha jimbo hilo linarudi CCM.
Lema alitoa maelezo hayo jana mbele ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa katika kesi ya kutaka
kuwatapeli viongozi wa Chadema.
Mbunge huyo alitoa ushahidi siku moja baada ya
Jaji huyo mstaafu kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo. Mbali ya Samatta
shahidi mwingine, Profesa Abdallah Safari alitoa ushahidi.
Kesi hiyo inamkabili Adam Abeid, ambaye wakati
kosa hilo linadaiwa kutendeka kwa kutumia simu, alikuwa ni mtahiniwa
binafsi (private candidate) wa mtihani wa Taifa wa kidato cha sita.
Lema, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alitoa
ushahidi wake juzi kwa kuongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Susan Kimaro.
Alisema mara tu baada ya kuvuliwa ubunge na
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha 2012, alipokea taarifa kutoka kwa John
Heche kuwa alikuwa akitafutwa na Wakili wa Chadema, Profesa Abdallah
Safari.
“Nilimtafuta Profesa Safari akaniambia natafutwa
na Jaji Samatta, akanipa namba yake nikampigia, lakini hakupokea
akanitumia ujumbe yuko kwenye kikao nitume meseji,” alidai Lema.
Lema alidai baadaye mtu huyo aliyejitambulisha
kama ‘Jaji Samatta’ alimtumia meseji akimpa pole kwa kuvuliwa ubunge na
kuahidi angemsaidia na kila alipojaribu kumpigia alikuwa akitaka
wawasiliane kwa meseji.
Aprili 12, 2012, Lema alidai kutumiwa meseji na
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa iliyokuwa imetumwa kwake na mtu
huyo aliyekuwa akijifanya Jaji Samatta ikisomeka:
“Mheshimiwa Slaa kesho nakwenda Dar kuonana na
Chande ili tufanye mazungumzo ana kwa ana tujue nini kitaendelea, hivyo
naomba unigharimie mafuta ya kwenda Dar.”
Lema alidai ujumbe huo ulimtia shaka kwamba
wanayewasiliana naye siyo Jaji Samatta, bali ni tapeli na kumtumia
meseji: “Wewe ni tapeli na tutakukamata.”
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment