Arusha
Home » » WAKULIMA MONDULI, KARATU SASA WAANZA KUTUMIA ZANA ZA KISASA

WAKULIMA MONDULI, KARATU SASA WAANZA KUTUMIA ZANA ZA KISASA

 
Zaidi ya wakulima 350 kutoka Wilaya za Monduli, Karatu na Simanjiro, wameanza kutumia zana za kisasa za kilimo baada ya kupatiwa mafunzo juu ya uelewa wa matumizi ya zana hizo na kuachana na kilimo cha jembe la mkono.
Hatua hiyo imeongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao yao.

Kauli hiyo ilitolewa na Meneja Mauzo wa kampuni ya Lonagro, Botwa Sanga, wakati wa semina ya siku moja iliyoendeshwa na kampuni hiyo katika kijiji cha Galapo, wilayani Babati.

Semina hiyo iliwakutanisha zaidi ya wakulima 250 kutoka maeneo mbalimbali mkoani Manyara.

Sanga alisema mafunzo hayo wameyatoa kwa nyakati tofauti kwa lengo la kuwaelimisha wakulima umuhimu wa kutumia zana za kisasa za kilimo, suala ambalo limesaidia kuinua kilimo chao kutoka kilimo kidogo hadi kilimo cha biashara.

‘’Tumewaelimisha na kuwafundisha umuhimu wa kilimo hifadhi kwa wakulima mbalimbali ili watumie vitendea kazi bora na kuleta tija katika kilimo,’’ alisema Sanga.

Aidha, alisema kampuni yake imekuwa ikitoa ushauri kwa wakulima wadogo kukopa zana za kilimo huku kampuni yake ikiwaunganisha na taasisi
mbalimbali za fedha hapa nchini zinazokubali kuwakopesha fedha ili wanunue zana hizo huku kampuni yake ikiwadhamini.

Alisema kwa kupitia mpango huo wa semina kwa wakulima ulioanza mwaka 2012, wakulima wengi wamebadilisha kilimo chao kutoka kilimo cha
jembe la mkono hadi kilimo cha kisasa, huku lengo ni kuwafikia wakulima wengi zaidi.

Wakulima Naasha Loyani, Jumanne Maboki na Hussein Juma, walisema kuwa kilimo walichokuwa wakikitumia cha kutumia jembe la mkono hakikuwanufaisha ila kwa sasa baada ya kuanza kutumia mashine za kilimo, wamenufaika zaidi.

Naye Meneja wa Lonagro, Ray Travas, alisema kampuni yake ambayo ni wakala wa
kampuni ya John Deere, alisema wamekuwa wakionyesha zana za kilimo kwa wakulima na kutoa ushauri ambao umesaidia kuleta tija kwa wakulima hao.

Alisema wamekuwa wakitoa elimu ya shamba darasa  ikiwa ni pamoja na utaratibu wa uendeshaji wa mashine za kilimo, matengenezo na utunzaji wa
mashine na usalama mahali pa kazi.

Kufuatia mafunzo hayo wakulima wengi wameweza kuwa na mwamko wa utumiaji wa zana za kisasa za kilimo huku baadhi yao wakitumia utaratibu wa kukodisha na wengine wakinunua kupitia mpango wa kukopeshwa.
CHANZO: NIPASHE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa