Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
ALIYEKUWA
Mgombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, (EALA), kwa tiketi ya
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Anthony Komu, ameibwaga
Serikali kwenye kesi aliyoifungua Mahakama ya Afrika Mashariki, (EACJ),
baada ya maombi yake mawili kukubaliwa huku moja likitupwa.
Mahakama hiyo, imesema kuwa kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania lilikiuka kipengele cha 50 (1) cha uanzishwa wa jumuiya ya
Afrika Mashariki kwenye uchaguzi uliofanyika Aprili 17, 2012.
Uamuzi huo wa shauri hilo namba 7/ 2012 la kutaka tafsiri ya
kipengele hicho, ulitolewa jana na Jaji Mkuu wa mahakama hiyo, Jean
Bosco Butasi kwa saa 1:20 kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 4:20 asubuhi
kwenye mahakama hiyo iliyopo jengo la makao makuu ya EAC, Arusha.
Alisema kuwa kitendo cha Bunge la Tanzania kutengeneza makundi manne
ya wagombea kwa kigezo cha jinsia, Zanzibar, vyama vya upinzani na
Tanzania Bara, ambayo wagombea wote walitokana na vyama vya siasa,
ulikinzana na kanuni ya 50 (1) ya mkataba wa uanzishwaji wa EAC
inayotaka kuwe na ushiriki wa makundi mbalimbali ya jamii.
Jaji huyo, alisema kuwa, pia kuruhusu mgombea kutoka chama cha siasa
cha Tadea, Lifa Chipaka kushiriki uchaguzi huo kutoka kundi la vyama vya
siasa wakati chama hicho kikiwa hakina uwakilishi bungeni ni kinyume na
kipengele hicho cha mkataba, huku akishauri kuwa angeweza kugombea
kupitia makundi mengine ndani ya jamii.
Aidha, mahakama hiyo ililionya bunge hilo kuhakikisha katika chaguzi
zake zinazofuata kuwa makini kuhakikisha mkanganyiko wa aina hiyo
haujirudii.
“Suala la kama wabunge wanaoiwakilisha Tanzania kwenye EALA
wamechaguliwa kihalali au hapana, litaamuliwa na Mahakama Kuu ya
Tanzania,” alisema Jaji huyo wakati akisoma uamuzi huo.
Aidha, aliuagiza upande wa wajibu maombi, Mwansheria Mkuu wa
Serikali, kumlipa mleta maombi, Komu robo ya gharama alizotumia kwenye
shauri hilo.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupa ombi moja lililowasilishwa
mahakamani hapo na Komu, akitaka kwa kuwa CHADEMA ni chama kikuu cha
upinzani, kilipaswa kupata nafasi kwenye bunge la EALA badala ya nafasi
hiyo kupewa vyama vyenye idadi ndogo ya uwakilishi wa wabunge.
Kwa upande wao mawakili wa Komu, Edson Mbogoro na John Mallya,
walisema wamerikidhika kwa uamuzi huo huku wakisema kuwa, sasa
wanajielekeza kwenye shauri walilolifungua Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.
Mallya, alisema kuwa kwenye shauri hilo namba 1/2012 litakalorudi
mahakamani hapo kwa ajili ya kupanga tarehe za kuendelea na usikilizwaji
Novemba 27 mwaka huu, wanaiomba mahakama hiyo itengue matokeo ya
uchaguzi wa wabunge wa EALA, kutokana na ukiukaji wa kanuni ikiwemo
kipengele cha 50 (1) cha mkataba wa uanzishwaji wa EAC.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Nkasari Sarakikya, aliyekuwa
akishirikiana na Pius Mboya na Mark Mukwamo, alisema kuwa wanasubiri
kupata nakala ya uamuzi huo waupitie ndipo waweze kujua nini cha
kufanya.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment