Home » » DIWANI AAHIDI KUPAKA RANGI MABATI YA SHULE

DIWANI AAHIDI KUPAKA RANGI MABATI YA SHULE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
DIWANI wa Kata ya Levelos, Ephata NanyaroDIWANI wa Kata ya Levelos, Ephata Nanyaro, (CHADEMA), amesema kuwa atapaka rangi kwenye mabati ya shule ya Msingi Levelos ili kuwawezesha wanafunzi kupata maji safi yanayovunwa nyakati za mvua.
Aidha, alisema kuwa hakuna mtu anayependa kufanya maandamano ila hufanyika pale haki za wananchi zinapokandamizwa, hivyo akawataka viongozi wa serikali jijini hapa kutimiza wajibu wako ili kuepusha mivutano isiyo na sababu.
Nanyaro, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati mfanyabiashara, Daniel Ole Materi, alipokuwa akikabidhi jengo la jiko la kisasa alilojenga shuleni hapo, ambako hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, (CCM).
Diwani huyo, alisema amekuwa karibu na uongozi na kamati ya shule kuibua na kusimamia miradi, kwa lengo la kuhakikisha wanaboresha mazingira ya shule hiyo ili yawavutie watoto kusoma na yachangie kuleta mabadiliko chanya, hivyo suala hilo lisichanganywe na siasa.
“Rotary Club wametusaidia kujenga matanki mawili kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua, kama mwalimu mkuu alivyokwisha waeleza, kwa sasa tatizo ni bati lina kutu hivyo maji yanayovunwa yanakuwa machafu, nadhani si busara kuwaomba tena waje watupakie rangi, hii nitaipaka mwenyewe…
“Niwashukuru wale wote wanaokuwa na moyo wa kusaidia shule hii, hata wale marafiki zangu waliosaidia kuchimba maji hapa shuleni, nawaomba na wengine wenye mapenzi mema wajitokeze tushirikiane kujenga bwalo la kulia chakula kwa ajili ya watoto wetu hawa,” alisema Nanyaro.
Kwa upande wake, mwekezaji huyo, Materi, alisema kuwa ataendelea kushirikiana na shule pamoja na jamii inayomzunguka kila atakapopata fursa ya kufanya hivyo ili kuzidi kujenga mahusiano mema, ambako pia alikabidhi magunia 12 ya mahindi kwa ajili ya kusaidia kuwapatia watoto uji nyakati za mchana.
Kwa upande wake mbunge Sendeka, aliahidi kutoa sh 500,000 kwa ajili ya kununulia masufuria ya kupikia shuleni hapo ikiwa ni miongoni mwa changamoto zilizoelezwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Elisante Kaaya, wakati akisoma risala.
Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela, aliipongeza shule hiyo kwa juhudi wanazoonyesha katika kuboresha mazingira yake, jambo alilodai shule nyingine jijini hapa zingekuwa na bidii hiyo, Arusha ingekuwa mbali.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa