Home » » MILIPUKO YA MABOMU:MMEFANYA NINI?

MILIPUKO YA MABOMU:MMEFANYA NINI?

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Wakati milipuko ya mabomu ikiongezeka nchini, hasa kwenye miji ya kitalii ya Arusha na Unguja, kumekuwa na sintofahamu miongoni mwa wananchi kuhusu Serikali kutotoa mkakati thabiti wa kupambana na tatizo hilo linalozidi kuota mizizi.
Si Wizara ya Mambo ya Ndani, ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Idara ya Usalama wa Taifa, Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama wala Jeshi la Polisi ambazo zimejitokeza kutoa mikakati ya kuwapa matumaini wananchi dhidi ya mashambulizi hayo ambayo yamekuwa yakilenga watu wa aina mbalimbali.
Jeshi la Polisi limekuwa likitoa taarifa za kawaida kuhusu milipuko hiyo, likisisitiza linadhibiti, lakini hali inaonekana kuwa mbaya zaidi hasa baada ya kutokea mlipuko mwingine mkubwa jijini Arusha uliojeruhi watu wanane, akiwemo mmoja ambaye alilazimika kukatwa mguu.
Wakati Mwananchi ikitafuta wahusika hao ili watoe mikakati ya kuzuia tatizo hilo, jana mchana Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliitisha mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia milipuko hiyo, akiwataka viongozi wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kuacha kutoa majibu mepesi na kuhakikisha wanadhibiti vitendo hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Arusha, Mbatia ambaye ni mtaalamu wa majanga kimataifa, alisema milipuko ya mabomu katika jiji hilo, Zanzibar na maeneo mengine nchini ni janga la Taifa lisilostahili kuachwa kuendelea.
“Siyo sahihi kwa viongozi na watendaji wa vyombo vya dola kutoa majibu mepesi kwa masuala magumu kwamba eti milipuko ya mabomu inasababishwa na masuala ya kidini, kisiasa au ushindani kibiashara,” alisema Mbatia.
“Mambo yanatokea nchini kana kwamba Serikali imeenda likizo. Damu inamwagika lakini hatuoni hatua madhubuti za kukomesha matukio haya. Viongozi wanaendelea na shughuli na ratiba za vikao na ziara kama vile hakuna kilichotokea,” alisema Mbatia.
Mbatia alizungumzia pia viongozi kukosa vipaumbele kwenye masuala muhimu huku akishangazwa na hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo kuhudhuria kikao cha Bodi ya Barabara jana, siku moja tu baada ya mlipuko wa bomu.
“Yaani bomu limelipuka Arusha jana (juzi), halafu leo (jana), Mkuu wa Mkoa hayuko ofisini eti anahudhuria kikao cha Bodi ya Barabara. Watu wanakufa, viongozi wanajadili kujenga barabara?” alihoji Mbatia
Kuhusu polisi
Alisema, “Ni aibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kujitokeza hadharani kutamba kuwa Jeshi la Polisi litahakikisha matukio ya milipuko ya mabomu yanakomeshwa, lakini yanaendelea kujirudia kila kukicha huku wakikimbilia kusema ni masuala ya kidini, ugomvi wa kibiashara na siasa,” alisema.
Alisema vyombo vya dola vinapaswa kuonekana vimeguswa na matukio haya kwa kuchukua hatua zinazoonekana kwa macho ya kawaida
“Baada ya Arusha kukumbwa na milipuko mara kwa mara, tulitarajia kuona helikopta za polisi, magari, pikipiki, farasi, mbwa na askari wa miguu wakifanya doria angani, barabarani na mitaani lakini ni tofauti,” alisema.
Kauli ya Chikawe
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe alisema matukio ya milipuko ya mabomu inayotokea Arusha hayahusiani na sababu za kisiasa, yanaweza kuwa ya kigaidi au uhasama wa kibiashara.
“Huu unaweza kuwa ni ugaidi. Magaidi nia yao ni kuharibu amani, kuua na kuumiza na kuiweka jamii katika woga tu na wala si jambo jingine labda uhasama wa kibiashara. Hakuna siasa katika hili hata kidogo,” alisema.
“Asikudanganye mtu, matukio hayo si ya kijambazi kwa sababu hakuna wanachochukua zaidi ya kuua. Hawachukui chochote wala hawamshikii mtu mtutu wa bunduki, ” alisema bila ya kueleza mkakati madhubuti wa kupambana na milipuko hiyo.
Badala yake, Chikawe alitaka jukumu hilo lifanywe kwa pamoja na wananchi.
“Polisi wanafanya kazi ya kuwatafua wahusika, wananchi hawana budi kutoa ushirikiano,” alisema waziri huyo.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi hakutaka Jeshi la Wananchi (JWTZ) lihusishwe na shughuli za uchunguzi na kukomesha matukio hayo ya kihalifu licha ya kuwa na wataalamu wa milipuko.
“Jeshi la Wananchi huitwa kwenye matukio kwa kuwa lina wataalamu wa milipuko, lakini Jeshi la Polisi ndilo linalohusika kufanya upelelezi,” alisema Waziri Mwinyi.
“Hata ripoti ya uchunguzi wa milipuko hiyo hupelekwa polisi na hivyo wao ndio wanaoweza kuzungumzia matukio ya milipuko.”
RPC, DC nao wajitenga
Kamanda wa polisi wa Arusha, Liberatus Sabas na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela walisema wanaotakiwa kuzungumzia matukio ya mabomu sasa ni timu iliyopo jijini Dar es Salaam

Tangu juzi, Sabas amekuwa akikataa kuzungumzia tukio hilo kwa maelezo kuwa litatolewa tamko na DCI Isaya Mngulu, huku Mongella ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Arusha, akisema Serikali imeunda kamati maalum kushughulikia matukio hayo ya mabomu.
“Suala hili limeundiwa ‘task force’ na ndiyo sababu sisi tupo kimya kwani Serikali inalifanyia kazi kwa umakini mkubwa,” alisema Mongella.
Kwa nini Arusha
Waziri Chikawe alipohojiwa ni kwa nini mashambulizi hayo yanatokea zaidi katika mkoa wa Arusha, alisema wahusika wamegundua kuwa mji wa Arusha ni rahisi kufanya ugaidi kwa sababu ya amani na utulivu wa muda mrefu.
Alisema Arusha ni mji ambao watu walijiaminisha kuwa wapo salama tofauti na Dar es Salaam, ndiyo maana wahalifu wengi sasa wanaulenga.
“Inawezekana kuwa uhalifu huo unasababishwa na mji kuwa karibu na Nairobi, lakini hilo si jibu la kumaliza tatizo hilo zaidi ya kuimarisha ulinzi na usalama ndani ya nchi yetu,” alisema.
Akijibu swali hilo, DCI Mngulu alisema: “Hawa wanalenga Arusha ili kusababisha tishio kwa wageni kwa kuwa ni mji wa utalii. Hii pia ndiyo inayotokea Zanzibar.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema suala hilo limetolewa ufafanuzi juzi na DCI Mngulu na kama yapo maelezo ya ziada basi aulizwe kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha.
Hata hivyo, DCI Mngulu alisema mikakati ya kuwapata wahusika waliolipua bomu katika mgahawa Arusha ni suala nyeti ambalo umma hautakiwi kulijua kwa sasa.
Alisema endapo jeshi la polisi litasema mipango inayofanywa au kutoa taarifa za taratibu zozote zile zinazofanywa basi maadui watapata mwanya wa kujificha au kutekeleza uhalifu mwingine baada ya kujua nini kinachofanyika.
Kamati ya Bunge
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Anna Abdallah alisema kwa sasa kamati hiyo haiwezi kuzungumza lolote zaidi ya kuangalia hali halisi ya usalama ilivyo nchini
“Tutachukua maoni ya wananchi na kile kilichopatikana kama kuna udhaifu wowote katika hili, sisi tutafikisha mbele ya Bunge,” alisema.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa