Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MBUNGE
wa Hai, Freeman Mbowe (CHADEMA), ametumia sh milioni 256.7 jimboni humo
kwa ajili ya kuchangia shughuli za maendeleo ambapo sekta ya elimu
imeongoza kwa kupata asilimia 37.76 ya fedha zote.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Katibu wa mbunge huyo, Ndonde
Totinan kwenye mkutano mkuu wa wilaya wa CHADEMA wakati alipotoa taarifa
ya utendaji wa ofisi ya mbunge kwa mwaka 2010 hadi Juni 30, mwaka huu.
Alisema ofisi hiyo ilizipatia fedha sekta nyingine za barabara, miti
na mazingira, afya, maji, vijana na kusaidia makanisa na misikiti.
“Katika fedha hizo sh milioni 125.8 zinatoka kwenye mfuko binafsi wa
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB) na sh milioni
130.9 zinatokana kwenye mfuko wa jimbo unaosimamiwa na mbunge huyo,”
alisema.
Totinan alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliobaki kabla ya
uchaguzi mwakani, Mbowe anatarajia kuwawezesha wananchi kuanzisha miradi
ya kuku, vikundi vya kuweka na kukopa (Saccos) ya vijana na kuboresha
shughuli za usafi wa mazingira.
Alisema sekta ya elimu ilitengewa sh milioni 96.9 ambapo kata zote 14
za Hai zilinufaika kulingana na ahadi alizotoa mbunge wakati wa
kampeni.
Alisema fedha hizo zilitumika kusaidia ujenzi wa madarasa, nyumba za
walimu, jiko, vyoo, kununua mashine ya kurudufisha (photocopy machine)
na ununuzi wa samani za ofisi kwenye baadhi ya kata.
Kwa mujibu wa katibu huyo, Mbowe alinunua trekta la sh milioni 70 kwa
ajili ya kusimamia programu ya miti na mazingira na shughuli nyingine
za kijamii ukiwemo ujenzi wa barabara na shule za jimbo hilo ambapo
linatumika pia kubeba taka kwenye soko la Kwa Sadala na Hai Mjini.
Upande wa barabara, Mbowe alitumia sh milioni 60.1 kwa ajili ya
ujenzi wa vivuko na madaraja kuhakikisha zinapitika kipindi chote cha
mwaka
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment