Home » » SPIKA EALA UTUPA HOJA YA KUMNG'OA

SPIKA EALA UTUPA HOJA YA KUMNG'OA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

SPIKA wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dk Magreth Zziwa, ametupa hoja ya wabunge wenzake kutaka kumng’oa akidai kuwa  suala hilo limekufa, hivyo haliwezi kujadiliwa ndani ya bunge hilo.
Hata hivyo, wabunge wanaompinga bado wamejipanga kuhakikisha hoja hiyo inaendelea kwani inakidhi vigezo kikanuni na hivyo kumshangaa kulitolea uamuzi suala linalomhusu.
Uamuzi huo wa spika unaenda kinyume na ushauri wa kisheria ulitolewa na mwanasheria wa EAC, Wilbert Kaahwa ambaye alisema hoja hiyo bado inakidhi vigezo vya kujadiliwa bungeni.
Zziwa alitoa uamuzi huyo juzi jioni kabla ya kuahirisha kikao cha bunge la bajeti, akisema kuwa alifikia uamuzi huo baada ya kupitia hoja zilizotolewa  na wabunge wakihoji kama hoja ya kumng’oa bado ni halali.
Alisema kuwa hoja ya kumng’oa haijawahi kuwasilishwa ndani ya bunge hilo kwani siku ilipotakiwa kujadiliwa ndipo mbunge, Fred Mbidde aliweka zuio la mahakama.
Kwa mujibu wa spika, hoja hiyo imezidi kukosa sifa hasa kutokana na hatua ya wabunge watatu wa Tanzania, Shyrose Bhanji, Adam Kimbisa na Maryam Ussi kuondoa majina yao kwenye orodha ya wanaounga mkono hoja hiyo.
Dk. Zziwa alisema kuwa anatumia kanuni ya 82 (2) inayompa mamlaka kuwa uamuzi wa spika ni wa mwisho kuhusiana na masuala yanayohusiana na ufafanuzi na matumizi ya kanuni za uendeshaji wa bunge.
Uamuzi huo ulipokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa wabunge wakati wale wanaomuunga mkono spika huyo wakionekana kufurahia kwa kupiga meza kisha kutoka nje na kuanza kukumbatiana kwa furaha.
Upande wa wabunge wanaompinga, walionekana kukasirishwa na hatua hiyo waliyodai kuwa ililenga kuamsha hasira miongoni mwao ili wasishiriki kupitisha bajeti ya jumuiya.
Wakizungumza na Tanzania Daima, wabunge Yves Nsabimana (Burundi) na Abdulkarim Harelimana(Rwanda) walisema kuwa wanachojua ni kwamba hoja hiyo ni halali na itaendele mpaka aliyeileta ndani ya bunge, Peter Muthuki (Kenya) atakapoamua kuiondoa.
Katika hatua nyingine, wabunge wa bunge hilo, wameipitisha kwa kauli moja bajeti ya jumuiya hiyo ya zaidi ya dola za Marekani milioni 124.07 kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Asilimia 59 ya fedha hizo itatumika kwenye miradi ya maendeleo huku asilimia 41 ikitumika kwenye masuala ya utawala.
Wabunge hao walipitisha bajeti hiyo jana mara baada ya kuijadili siku nzima ya juzi na jana kupata majibu kutoka kwa katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera na Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, Shemu Bageine, waziri kutoka Uganda.
Chanzo:Tanzania Daima 

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa