Home » » LOWASSA:TUNAWEZA KUWA KINARA WA UCHUMI

LOWASSA:TUNAWEZA KUWA KINARA WA UCHUMI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

WAZIRI Mkuu mstaafu ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, mkoani Arusha, Bw. Edward Lowassa, amesema Tanzania inaweza kuwa kinara wa uchumi Ukanda wa Afrika Mashariki kama utajiri wa rasilimali na amani iliyopo vitatumika vizuri.

Bw. Lowassa aliyasema hayo Mjini Dodoma juzi kwenye semina ya wabunge iliyoandaliwa na Asasi za Kiraia nchini AZAKI na kusisitiza kuwa, utajiri waamani na rasilimali zilizopo ni vitu vinavyoweza kuifanya Tanzania kuwa kinara katika eneo hili.

"Tanzania tuna bahati kubwa ya kuwa na vitu ambavyo wenzetu hawana hususan amani... wenzetu hawana amani kama tuliyonayo, amani hii inatoa nafasi ya kuweza kufanya biashara na shughuli nyingine za kiuchumi bila wasiwasi," amesema Bw. Lowassa.

Alisema rasilimali nyingi zilizopo kama gesi na madini, kama zitatumika vizuri, zitakuza uchumi wa nchi kwa kiwango kikubwa ambapo kama kutakuwa na mgawanyo sawa wa matumizi ya rasilimali hizo, Taifa litakuwa na uwezo wa kujiimarisha kielimu na miundombinu.

Bw. Lowassa ambaye alikuwa Mwenyekiti katika semina hiyo ambapo wachangiaji wengi walieleza wasiwasi wao wa jinsi Tanzania inavyoweza kuingia katika soko la ushindani la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Mimi nasema kuwa, Tanzania tunaweza kuongoza katika soko la ushindani Afrika Mashariki... hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kama changamoto hizi zitafanyiwa kazi," alisema Bw. Lowassa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje ya Bunge.

Semina hiyo iliandaliwa ili kuwapa ufahamu wabunge juu ya shughuli na changamoto ambazo asasi hizo za kiraia inakabiliana nazo ambapo asasi hizo pia zinafanya Maonesho katika Viwanja vya Bunge yakihusisha kazi za mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa