Home » » NDC KUJENGA KIWADA ZIWA NATRONI

NDC KUJENGA KIWADA ZIWA NATRONI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Bonde la EngarukaSHIRIKA la Maendeleo la Taifa (NDC) limeanza mchakato wa kupata wazabuni kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya uzalishaji magadi soda kwenye Ziwa Natron na Bonde la Engaruka.
Viwanda hivyo vitajengwa umbali wa zaidi ya kilometa 10 kutoka kwenye ziwa yatakapochimbwa magadi ambapo wanatarajia kuzalisha tani za ujazo milioni 1.5 kwa mwaka, huku thamani yake kwa bei ya soko ikiwa zaidi ya sh bilioni 720.
Kiwanda kitakachojengwa Ziwa Natron, ndicho kitaanza kutekelezwa ambapo kinatarajiwa kukamilika ifikapo mwanzoni mwa 2015 na utafiti pekee umegharimu sh bilioni 2.5.
Akizungumza juzi jijini hapa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Mlingi Mkucha, alisema kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kukamilika kwa utafiti wa kina wa mazingira ambao pamoja na mambo mengine umethibitisha kuwa hakuna madhara yoyote kwa mazalia ya korongo wadogo (Lesser Flamingo) wanaoishi kwenye maeneo hayo kama ilivyokuwa ikihofiwa na wanamazingira.
Mkucha alisema kuwa watafiti hao walijikita katika kuangalia namna uzalishaji wa magadi soda utakavyoweza kufanyika bila kuathiri mazingira kwenye maji, hasa mchanganyiko wa maji na kemikali usiharibike, ubaki kama ulivyo sasa.
Kwamba korongo wadogo wanaozaliana na kuishi kwenye Ziwa Natron waliwachunguza maisha yao hatua kwa hatua kwa kipindi cha mwaka na kuona hakuna madhara yoyote yatakayowapata.
Alisema kuwa kulingana na ujazo wa magadi soda yaliyopo kwenye maeneo ya Ziwa Natron na bonde la Engaruka, yanaweza kuvunwa kwa miaka 540 bila kuisha, huku akisema kuwa muda huo utaongezeka kwani kila mwaka magadi hayo huongezeka mita za ujazo bilioni 1.9.
Mkucha aliongeza kuwa tayari mchakato wa kuandaa mpango bora wa ardhi kwenye maeneo hayo umeanza ili kuainisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya watu, viwanda, biashara na huku wakala wa barabara nchini (Tanroads) akitakiwa kuangalia barabara zinazoelekea maeneo ya mradi pamoja na njia za reli.
“Tumekuja kushauriana na viongozi wa wilaya za Monduli na Longido pamoja na mkoa ili miradi hii ifanyike kwa muda tuliojiwekea, baada ya muda mfupi mtaanza kuona mabadiliko makubwa, kutakuwa na ajira za moja kwa moja si chini ya 1,000.
“Viwanda hivi vya magadi vitavuta viwanda vingine kujengwa kwenye maeneo haya kwa ajili ya kutumia magadi kama malighafi, ndiyo sababu katika utengaji wa maeneo kutatengwa maeneo ya viwanda, watu wa mabenki nao watakuja, migahawa, wote hawa watatoa ajira,” alisema Mkucha.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli lilipo Ziwa Natron, Jowika Kasunga, alisema kuwa wananchi wameshirikishwa kiasi cha kutosha, na kwamba baada ya matokeo ya utafiti watawaeleza watu namna watakavyonufaika na mradi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Longido lilipo bonde la Engaruka, James ole Millya, alisema kuwa hana taarifa za wananchi kuupinga mradi huo, huku akisisitiza kwamba wananchi wa Kitongoji cha Oasis wanaoishi kandokando ya bonde hilo wako tayari mradi huo uanze mara moja.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa