Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MSHINDI katika mbio za kilomita 10 Sokoine Mini Marathon
zinazofanyika Monduli Juu wilayani Monduli mkoani hapa, anatarajiwa
kuondoka na kitita cha sh 500,000.
Kwa mujibu wa mratibu wa mbio hizo, Wilhelm Gidabuday, zitahusisha
pia walemavu sambamba na michezo mingine ikiwemo ya kuruka chini na
kurusha mkuki.
Alisema kuwa kwa upande wa mbio za kilomita 10 zitakazohusisha watu
wazima wasio na ulemavu, mshindi wa kwanza atazawadiwa kitita cha sh
500,000, wa pili sh 400,000 huku wa tatu akijipoza na sh 300,000 kwa
wanaume na wanawake.
Gidabuday alisema kuwa watakaofanikiwa kushika nafasi ya nne watapata
sh 100,000 na wa tano sh 75,000 huku mshindi wa sita akifutwa jasho
kwa sh 50,000.
“Hizo ndio zawadi kwa washindi wa mbio ndefu za kilomita 10 kwa mwaka
huu, kuanzia wa kwanza hadi wa sita, lakini kwa wale watakaoshindwa
hatuna cha kuwapa, zaidi ya kuwatia tu moyo waendelee kukimbia kwa mara
nyingine mwakani, kwani wakikazana watashinda huku pia wakitambua kuwa
lengo ni kumuenzi aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Sokoine,” alisema.
Mbio hizo kwa upande wa walemavu mshindi wa kwanza atajinyakulia sh
200,000 wa pili sh 150,000 huku mshindi wa tatu akiondoka na sh
100,000.
Kuruka chini mshindi wa kwanza atajinyakulia sh 200,000 na wa pili sh
150,000 huku mshindi wa tatu akijipoza kwa sh 100,000 hivyo hivyo
katika kurusha mkuki.
Mbio hizo ni sehemu ya matukio yatakayoadhimisha miaka 30 ya kifo cha
aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine.
Maadhimisho hayo yatakayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, pia
yatahudhuriwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa na
viongozi wengine mbalimbali, ambapo pia kutakuwa na misa maalumu ya
kumuombea hayati Sokoine
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, Rais Kikwete atawasili leo mkoani hapa.
Mbio hizo zitaanza kuanzia saa moja kamili asubuhi na kuisha saa nne,
ambapo watu wote watakwenda kanisani kwa ibada maalumu na baadaye rais
ataongoza msafara hadi nyumbani kwa familia ya hayati Sokoine, yalipo
makaburi na kuweka mashada ya maua.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment