Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MAHABUSI wa Gereza Kuu la Arusha wamevua nguo hadharani katika Mahakama ya Mkoa kwa kile wakishinikiza kesi zao kusikilizwa haraka.
Hali hiyo ilijitokeza juzi na kusababisha baadhi ya ndugu wa mahabusi hao waliokuwa mahakamani hapo kusikiliza kesi, kukimbia kuepuka kushuhudia ndugu zao wakivua nguo.
Walikaririwa wakilalamikia Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Idara ya Upelelezi ya Mkoa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Arusha juu ya ucheleweshaji usikilizwaji wa awali wa kesi zao.
Mahabusi hao, wengi wakiwa ni wenye kesi za dawa za kulevya , wizi wa kutumia silaha na mauaji, walidai wamekaa mahabusu zaidi ya miaka miwili bila kusomewa maelezo ya awali katika kesi zao huku wakiendelea kuteseka gerezani.
Awali kabla ya kuvua nguo, walipofikishwa juzi mahakamani saa 3.15 asubuhi wakiwa ndani ya basi la Magereza lenye namba za usajili MT 0041, waligoma kushuka wakitaka kupewa maelezo ya kujitosheleza kutoka kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha juu ya malalamiko yao.
Askari magereza waliomba kuongezewa idadi na ndipo askari zaidi ya 15 waliletwa wakiwa kwenye gari aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili MT 0075.
Baada ya mahabusi kuona ulinzi umeimarishwa huku basi lao likiwa limezingirwa na askari Magereza wenye silaha za moto, waliamua kuvua nguo zote huku wakiimba na wengine wakipiga kelele za kutaka kufahamu hatma ya kesi zao.
Akizungumzia suala hilo jana, Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Willberd Mashauri alisema hakuwepo mahakamani.
Alisema alikuwa katika vikao vya Mahakama Kanda ya Arusha.
Hata hivyo alikiri malalamiko ya mahabusi hao kuwepo na kwamba yanafanyiwa kazi. Agosti mwaka jana, mahabusi hao pia waligoma kushuka kwenye basi lao wakishinikiza kesi zao zianze kusikilizwa.
Chanzo:Habari Leo
0 comments:
Post a Comment