Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
RAIA wa kigeni wameshutumiwa kuwa sehemu ya ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kupachika mimba wanawake wa kitanzania na kuwatelekeza. Hayo yameelezwa na mratibu msaidizi wa kituo cha kulelea watoto waishio katika mazingira magumu cha Samaritan Village Tanzania, Agnes Mtui kilichopo eneo la Moshono jijini Arusha.
Mratibu huyo alikuwa akizungumza wakati wa kupokea misaada ya kibinadamu kutoka kwa kampuni ya uagizaji na usafirishaji wa vifurushi nchini ya Next Couriers and Logistics.
Agnes akimzungumza mtoto mmoja kati ya 30 wanaolelewa kituo hapo Sundey Samaritan (1) mwenye asili ya kiasia ambaye alieleza kuwa kabla ya kufikishwa katika kituo hicho aliokotwa nje ya kiwanda cha kutengeneza vyandarua na fulana cha AtoZ kilichopo Kisongo jijini hapa.
Akimuelezea mtoto huyo alisema aliokotwa na majirani wa kiwanda hicho akiwa na muda wa wiki moja tangu kuzaliwa na kisha walipatiwa taarifa na kwenda kumchukua na kumpatia huduma ya kwanza katika hospitali ya Mount Meru kisha kumlea katika kituo hicho mpaka sasa.
Alisema mbali na mtoto huyo tayari walishawahi kulea watoto wengine wawili yenye asili ya kiasia ambao alidai waliokotwa katika maeneo tofauti tofauti wakiwa wametupwa na wazazi baada ya kupewa mimba na rai wa nje.
“Kwa hiyo kutokana na hili tunaona hata hawa wenzetu wanahusika katika kuwapachika mimba wasichana wa kitanzania halafu wanawatelekeza, jambo ambalo linachangia kia katika kuongeza tatizo hili sasa serikali ilitambue na hili,”alisema Agnes.
Aidha aliitaka jamii ya watu hao kujitoa katika kuchangia kukabiliana na tatizo hili, lakini pia kujitokeza katika kusaidia kundi hili la watoto hao na kuwatambua pia.
Akizungumzia changamoto wanazokumbana nazo alizitaja kuwa ni ukosefu wa ada za watoto wanaowasomesha katika shule mbalimbali, vifaa vya shule, ukosefu wa vyumba vya joto kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda na kisha kutupwa, chakula pamoja fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa hospitali ya kituo hicho.
Hivyo akaiomba serikali kuchukua jukumu la gharama kwa ajili ya watoto wanaopelekwa kwenye vituo mbalimbali hapa nchini kutokana kuwepo changamoto kubwa na mwamko mdogo na hata kukosekana kwa wafadhili katika vituo hivyo.
Akizungumza kituoni hapo wakati wa kukabidhi misaada hiyo mhasibu wa Next Couriers kanda ya kaskazini Kelvin Lyimo alisema kampuni yake imeamua kutoa msaada huo wa vyakula kama mchele, sukari, unga wa sembe, mafuta ya kula na sabuni za kuongea vyenye thamani ya Sh 500,000 kama njia ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na kituo hicho.
Kituo cha Samaritan kilianza kazi hiyo tangu mwaka 1996 chini ya wafanyakazi 13 na tayari kimeshalea watoto zaidi ya 70 huku watoto 40 wakiwa wameasiliwa na watu mbalimbali toka ndani na nje ya nchi.
Chanzo:Habari Leo
0 comments:
Post a Comment