Arusha
Home » » Wananchi watishia kuwachoma moto wastaafu wa JWTZ

Wananchi watishia kuwachoma moto wastaafu wa JWTZ

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Zaidi ya wakazi 300 wa kitongoji cha Olmapinuu katika kijiji cha Bwawani  wilaya ya Arumeru,  juzi waliwashikilia kwa saa sita askari  wanne wastaafu wa Jeshi la Wananchgi wa Tanzania (JWTZ) wakiwa na trekta lao wakidai kuwa wamevamia eneo la shamba la wanakijiji hao.
 Wananchi hao waliwatishia wastaafu hao kuwa watawateketeza kwa moto endapo wataendelea kulima shamba hilo.

Sakata hilo la ni mwendelezo wa migogoro ya ardhi wilayani Arumeru.

 Hata hivyo, lilimalizika kwa amani baada ya viongozi wa Halmashauri ya Arusha Vijijini wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Bwawani,  Lazaro Orasirasi, kuingilia kati na kuwapoza wananchi hao ambao walikuwa wamejiandaa kwa shari wakiwa na silaha za jadi za aina mbalimbali.

Kwa upande wao, wanajeshi hao wastaafu walidai kupewa shamba hilo kihalali na mamlaka zinazohusika.

Walifika shambani hapo wakiwa na trekta lenye namba za usajili T 814 CDZ huku wakiwa na bunduki tatu aina ya rifle tayari kwa lolote.

Mmoja wao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema walipewa eneo hilo mwaka 2012 lakini tangu wakati huo wameshindwa kufanya lolote kutokana na wananchi  kudai kuwa eneo hilo ni lao walilopimiwa na kumilikishwa kihalali na kufuata taratibu zote za kisheria.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Saanay Mesiaki, aliwaambia waandishi wa habari waliofika katika shamba hilo kuwa wamekuwa wakiishi katika eneo hilo kwa miaka zaidi ya 50 na mwaka 2005 walichangishwa Shilingi milioni tatu kwa ajili ya kupimiwa eneo hilo lakini tangu wakati huo hawajapewa hati yoyote zaidi ya kuona kwamba wanavamiwa na wastaafu hao.

"Sisi tumezaliwa na kukulia hapa na tumezika wazazi wetu na hata mababu zetu hapa na tulichangishwa Shilingi  milioni tatu na kutoa mbuzi saba kwa ajili ya kupimiwa eneo hili, sasa hawa wanaotuvamia na mabunduki wametoka wapi na wanataka nini hapa?,” Alihoji.

Aliongeza:  "Baada ya eneo letu kuvamiwa tulilalamika hadi wilayani kwa mkuu wa wilaya na amri tuliyopewa ni kwamba sote (sisi na  wavamizi), tusifanye lolote hadi ufumbuzi wa suala hilo utakapopatikana.

Sasa tunashangaa wenzetu wanakuja na matrekta na bunduki…sisi hatuogopi na tuko tayari kufa kwa ajili ya eneo letu," alisisitiza Mwenyekiti huyo huku akishangiliwa na wananchi.

“Hatutaki damu imwagike hapa lakini pia tueleweke kwamba tunadai haki yetu na kamwe hatutishwi na lolote wala hatumwogopi yeyote,” alisema.

Alisema kwamba wanajeshi hao wastaafu 30 waliingia katika shamba hilo bila kufuata taratibu kwa kuwa si serikali ya kijiji wala kitongoji iliyopewa taarifa zozote za ujio wa wao.

Alisema kwamba shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 708.9 ambalo awali lilikuwa linamilikiwa na Kampuni ya Lucy Estate, ni mali  halali ya wananchi wa kitongoji hicho ambao ni wafugaji wa Kimasai.

Aliongeza kuwa uamuzi wa wananchi hao kuwaweka chini ya ulinzi wanajeshi wastaafu  hao na trekta lao, umetokana na hatua walizochukua mwaka jana ambapo wanadaiwa kufyeka ekari 35 walizolima wananchi hao zikiwa na mahindi na ngwara na kuwasababishia ukosefu wa chakula bila sababu yoyote.

Akizungumza na wananchi hao, Diwani Orasirasi ambaye alifuatana na baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo, alithibitisha wananchi hao kuchangishwa kwa ajili ya upimaji wa eneo hilo, lakini akasema kuwa taratibu za kisheria bado hazijakamilika ili kuwakabidhi eneo hilo.

Hata hivyo, alipoulizwa kuwa ilikuwaje kuwachangisha wananchi kupimiwa eneo ambalo lina mmiliki halali kisheria, Diwani huyo hakujibu swali hilo zaidi ya kusema kwamba taratibu za kisheria zinaendelea ikiwa ni pamoja na kumshawishi mmiliki huyo kuwagawia wananchi sehemu ya shamba hilo.

Migogoro ya ardhi wilayani Arumeru imekuwa ni tatizo sugu kutokana na wamiiliki wachache wa mashamba makubwa kuhodhi eneo kubwa huku wananchi wakikabiliwa na uhaba wa ardhi.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa