MBUNGE
wa Longido Lekule Laizer (CCM), amewashauri wafugaji nchini kuachana na
ufugaji wa kienyeji na kuanza kufuga kisasa ili kuongeza thamani ya
mazao ya mifugo yao.
Ushauri huo ameutoa hivi karibuni wakati
akizungumza na wanachama wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) katika
mkutano ulioandaliwa na chama hicho ili kuwashukuru baadhi ya wabunge
waliofanikisha kukomesha operesheni mbalimbali zilizokuwa zikiua mifugo
yao.
Alisema kuwa wafugaji wengi nchini wamekuwa wakifuga mifugo
isiyokuwa na tija kwa kufuga ng'ombe ambao mbegu zao ni ndogo hivyo
kupata fedha kidogo kutokana na ufugaji wa aina hiyo hivyo kuwashauri
kuachana na ufugaji huo na kuanza kufuga kisasa kwa kutafuta mbegu nzuri
za madume ya ng'ombe ambayo zinakuwa kwa haraka na pindi zinapopelekwa
sokoni huweza kuuzwa kati ya sh. milioni 1.5 hadi milioni 2.
Aidha
aliwataka wafugaji hao kuheshimu maeneo ya wakulima ili kuepusha
migogoro ambayo kwa siku za hivi karibuni imesababisha ugomvi na mauaji
na kusema kuwa hata kama Serikali itatenga maeneo ya wafugaji kama
hawataheshimiana na kujua mipaka yao ni lazima migogoro hiyo itaendelea
na kuzidi kuhatarisha amani ya wafugaji nchini.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa bodi ya wafugaji kutoka kanda ya Ziwa Venance Kabwebwe
aliwalaumu watendaji wakuu wa Serikali wenye dhamana na wafugaji kuwa
ndiyo chanzo cha migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kuwa hawana msaada
wowote katika kukabiliana na migogoro hiyo pindi wanapopata taarifa kwa
kushindwa kuitatua kwa haraka.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment