WATAALAMU,
wadau wa mawasiliano na maofisa kutoka nchi 25 wanachama wa Jumuia ya
Madola wanakutana jijini hapa kwa siku nne kuanzia jana kujadili
harakati za uzimaji wa mitambo ya analojia katika nchi zao na kuingia
katika mfumo wa digitali.
Mkutano huo umeandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Jumuia ya Madola
inayojihusisha na masuala ya mawasiliano, Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) na Taasisi ya Mawasiliano kwa nchi za Afrika Mashariki
(EACO).
Wakizungumza na waandishi wa habari jana kabla ya kuanza kwa mkutano
huo, maofisa kutoka taasisi hizo tatu wenyeji wa mkutano huo, walisema
mkutano huo ni muhimu kwa mataifa hayo ambapo yanalazimika kuzima
mitambo ya analojia ifikapo Desemba mwakani.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mawasiliano
Jumuia ya Madola, Profesa Tim Unwin, alisema lengo kuu la kuwakutanisha
wadau wa sekta ya mawasiliano ni kuangalia changamoto mbalimbali
zilizopo katika uzimaji wa mitambo ya analojia na jinsi ya kukabiliana
nazo.
Mkurugenzi wa Utangazaji wa TCRA, Habbi Gunze, alisema Tanzania
ambayo tayari awamu ya kwanza ya uzimaji mitambo imeishafanyika,
kinachosubiriwa ni taarifa ya tume iliyoundwa kuchunguza changamoto
zilizojitokeza katika awamu hiyo, ili zifanyiwe kazi na awamu ya pili
iweze kutangazwa.
Alitaja baadhi ya changamoto ni uwepo wa ving’amuzi vichache kukidhi
mahitaji na kupungua kwa matangazo ya biashara katika vituo vya luninga
baada ya kuzima mitambo ya analojia.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment