Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole (katikati)
akizungumza katika mkutano wa utekelezaji wa ilani ya chama hicho Kata
ya Monduli Mjini ambapo alionya watu kuacha kumfuatafuata Mbunge wa
Monduli, Edward Lowassa. Kulia ni katibu wa Uenezi Mkoa, Isack Joseph na
kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Reuben Ole Koney.
Mpasuko ndani ya CCM unazidi kuongezeka baada ya viongozi wa
chama hicho Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Monduli kuibuka na kukemea
‘siasa za vitisho na hofu’ dhidi ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole
Nangole, akiambatana na Mwenyekiti wa Wilaya ya Monduli, Reuben Ole
Kuney na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Isaack Joseph alieleza
kuchoshwa na kauli za vitisho dhidi ya Lowassa zinazotolewa na baadhi ya
viongozi wa chama hicho, wakati wanachama wote ni sawa na hakuna mwenye
ukubwa mithili ya tembo wa kumtisha mwenzake.
Kauli ya kiongozi huyo, imekuja siku mbili baada
ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kukemea vitendo vya rushwa kwa
watu wanaotaka kuwania urais na kuiagiza Kamati ya Maadili ya chama
hicho inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula
kuwashughulikia.
Akizungumza katika mkutano wa utekelezaji wa Ilani
ya uchaguzi katika Kata ya Monduli Mjini ambao pia ulienda sambamba na
maadhimisho ya miaka 37 ya CCM, Nangole alisema wanachama wote wa CCM
wana haki sawa na hakuna wa kuogopwa kama tembo, wala mdogo wa
kunyanyaswa kama sisimizi, ili mradi hakuna ambaye anavunja sheria na
taratibu za chama hicho.
“CCM ni yetu sote, hakuna mtu wa kuogopwa kama
tembo wala sisimizi, mimi binafsi sijaona kosa alilofanya Lowassa hadi
sasa. Kwa nini wanamfuatafuata na kumshambulia kupitia vyombo vya
habari?” alihoji Nangole.
Alisema anawashangaa baadhi ya viongozi kuanza
kutoa kauli za kumshambulia Lowassa na kumtishia kumpeleka katika Kamati
ya Maadili ya chama hicho kwa tuhuma kuwa, ameanza kampeni za urais,
jambo ambalo sio kweli, kwani tangu mwaka 1993 amekuwa akiendesha
harambee mbalimbali na amekuwa akifanya sherehe kila mwaka nyumbani
kwake.
“Nakumbuka Rais Jakaya Kikwete mwenyewe
alihudhuria sherehe nyumbani kwa Lowassa mwaka 2006 na alimpongeza kwa
sherehe hiyo kwa kuwaalika marafiki zake wengi na kupokea mwaka mpya,
lakini nashangaa sasa sherehe yake kuwa nongwa,” alisema Nangole.
Alisema anaamini kuna ajenda ya siri dhidi ya
Lowassa, kwani hata makada wengine wa chama hicho wameonyesha nia ya
kuwania urais, lakini hakuna ambaye anawasema.
“Kwani hatujuani? Tunajuana, wapo wanaopita
wanasema hawajaoteshwa wanangoja kuoteshwa, wengine wanasema afya zao
nzuri na wanaweza kuongoza miaka mitano, wengine wamesambaza kalenda
nchi nzima na wengine wanapigiwa kampeni na viongozi wa juu wa chama,
lakini hakuna anayesemwa zaidi ya Lowassa,” alisema Nangole.
Nangole alisema wao wanajua taratibu za chama, hivyo hawawezi sasa kuanza kampeni kabla ya muda mwafaka.
Alisema Tanzania ni ya watu wote na waliongia CCM
ni kutokana na kuwa na imani ya chama hicho, hivyo hakuna sababu za
ubabe na baadhi kujiona bora zaidi ya wengine.
Alisema Lowassa tangu mwaka 1993/4 alipokuwa
waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, alianza utaratibu wa harambee
kusaidia wazazi waliokuwa na watoto wanaokosa nafasi ya shule na
kuanzisha mifuko na alikuwa akienda kanisani na misikitini, iweje leo
iwe nongwa?
“Mungu amempa uwezo akisimama watu humfuata nyuma katika
kusaidia wanyonge, yeye ana nguvu za Mungu, nadhani hiyo ndiyo inamletea
taabu. Sasa mimi niulize kuna kamati za maadili sawa, tangu mwaka 1993
ameanza harambee leo wanasema ameanza kampeni?” alihoji Nangole.
Alisema Lowassa amekuwa akisaidia kila pembe ya
nchi katika nyumba za ibada na hafanyi kampeni, kwani hao wanaosaidiwa
siyo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM.
Amshambulia Malecela
Alisema anamheshimu sana Makamu Mwenyekiti mstaafu
wa chama hicho, John Malecela na alidhani angetumia busara zake
kumsaidia Rais Kikwete ili kukabiliana na matatizo ya kijamii kuliko
kuibua suala la fulana za kuashiria Lowassa ameanza kampeni.
“Tuna matatizo ya ajira, elimu, afya, ajali, rais
anahangaika usiku na mchana, ningedhani huyu mzee mwenye umri mkubwa
ameongoza nchi kama Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa
CCM, angemshauri Rais kwani tuna matatizo mengi kuliko fulana. Mimi
nadhani busara zake zingesaidia taifa kuliko fulana ambazo hata
wanamichezo wanapewa. Nimesikitika sana,” alisema Nangole.
Nangole amekuwa mwenyekiti wa tatu wa CCM mkoa
kujitokeza hadharani na kutoa matamshi ya kutetea kinachoelezwa kama
mienendo ya Lowassa.
Wengine ni Khamis Mgeja wa Shinyanga na Mgana
Msindai wa Singida wanaoungana na wabunge, John Komba wa Mbinga
Magharibi na Beatrice Shellukindo wa Jimbo la Kilindi.
Lowassa asiwe na hofu
Kwa upande wake ole Kuney alisema anashangaa watu
wanaomshambulia Lowassa bila sababu za msingi hasa kuhusiana na mbio za
urais ambazo hata hajatangaza.
“Mbona watu wengi wanasema wanataka kugombea na
wanajulikana, mbona hawasemwi. Tunamwomba Lowassa asiwe na hofu awapuuze
hawa watu, wanatapatapa kama wafamaji,” alisema Ole Kuney.
Alisema lazima ijulikane Lowassa ana watu, ana marafiki wa kila aina, kwa hiyo akizunguka na wajasiriamali hakuna tatizo.
Chanza;Mwananchi
Chanza;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment