Home » » Lema Vs Polisi tena Arusha

Lema Vs Polisi tena Arusha

Mbunge wa Arusha, Godbless Lema.
 
Polisi mkoani hapa, imetoa notisi ya kukamatwa kwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema (pichani) na wenzake watatu ili kuhojiwa kuhusu malalamiko ya vurugu zilizotokea kwenye mikutano ya kampeni za uchaguzi wa kiti cha udiwani Kata ya Sombetini, wiki iliyopita na kusababisha watu kadhaa walijeruhiwa.
Hata hivyo, Mbunge Lema alisema jana kuwa hana taarifa ya kutafutwa polisi kwa ajili ya mahojiano.

Alisema kama ni kweli anatafutwa basi taratibu zifuatwe ili aweze kwenda kuripoti polisi.

Alisema anachofahamu ni kwamba ofisi ya Kamanda wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha ilimtaka kuwapata taarifa wanachama watatu wa Chadema ambao walikuwa wakihitajika kwa mahojiano.

Aliwataja wanachama hao kuwa ni Anorld Kamde, na wengine kwa jina moja moja tu la Frank na Daud.

Aidha Kamanda Sabas alisema maandamano yaliyopangwa na Chadema kufanyika leo yamepigwa marufuku kwa maelezo kuwa madai yao yanashughulikiwa.

“Tumewaandikia barua Chadema kuwa madai yao yanashughulikiwa hivyo sio vema kufanya maandamano wakati mambo yao yakifanyiwa kazi,” alisema.

Chadema ilipanga kufanya maandamano leo wakitaka polisi iwakamate watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM ambao wamekuwa wakiwafanyia vurugu na kuwaumiza wanachama wao kwenye mikutano yao ya  kampeni za uchaguzi wa udiwani Kata ya Sombetini.

Akizungumzia kuhusu maandamano yao, Lema alisema wameamua kusogeza mbele hadi Alhamisi wiki hii kwa kuwa baada ya kuwasilisha barua yao ilibainika kuwa CCM nao waliomba kufanya maandano yao leo.

Nao CCM kwa upande wao wamewasilisha malalamiko polisi wakiwashutumu Chadema kuwafanyia vurugu na kuwajeruhi wanachama wao.

Kamanda Sabas alisema tayari ofisi yake imekwishawahoji wanachama kadhaa wa CCM wanaolalamikiwa na Chadema kuhusu vurugu hizo, na sasa wanahitaji kuwahoji wanachama watatu wa Chadema pamoja na Mbunge Lema kufuatia malalamiko ya CCM.

“Tumewapa notisi wanachama Chadema waje kuhojiwa, lakini tunaambiwa hawawezi kuhojiwa hadi kibali cha Katibu Mkuu (Dk Willbrod Slaa), alisema na kuongeza, “tunataka waje tuwahoji.”

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema jana kuwa notisi ya kukamatwa kwa Lema na wenzake ilitolewa kuanzia Jumamosi iliyopita.

Alisema tangu wakati huo hadi leo (jana) Lema na wenzake ambao Kamanda hakutaka kuwataja walikuwa bado hawajaenda kuripoti polisi.
“Tulitazamia leo angekuja kuripoti lakini mpaka muda huu hajaonekana,” alisema na kuongeza “tukiwahoji tutapeleka mashataka hayo kwa Mwanasheria Mkuu ambaye kwa mujibu wa sheria ndiye anayefungua mashtaka.”

Uchaguzi wa udiwani Kata ya Sombetini ulianza kukumbwa na vurugu wiki iliyopita baada wanachama watatu wa Chadema kujeruhiwa vibaya na watu wanaodaiwa kuwa ni kikundi cha ulinzi cha CCM.

Mwenyekiti wa Chadema wilayani Arusha, Ephata Nanyaro, aliwaeleza waandishi wa habari wiki iliyopita kuwa matukio hayo yalitokea Januari 20, mwaka ambapo licha ya wananchama wao kuumizwa lakini  jeshi la polisi liliwakamata na kuwageuzia kesi kuwa wao ndiyo waliofanya vurugu.

Alisema siku hiyo majira ya saa nane mchana  mwanachama wao, Vitalis Bernad  alipigwa shoka la kichwa na kijana aliyedai kuwa ni kiongozi wa CCM wakati akipita maeneo ya kona ya Mabuda  akiwa kwenye pikipiki yenye bendera ya Chadema wakielekea kwenye mkutano wa mgombea wa chama chao, Ally Bananga.

Alisema kwa bahati nzuri Barnad alikuwa amevaa kofia ngumu za waendesha pikipiki hivyo hakuumia sana lakini watu walikuwa pale walijaribu kumkimbiza mhusika lakini hawakufanikiwa kwani alikimbilia kwenye ofisi ya CCM ambapo walitokea kundi la watu wenye mapanga kutoka ndani ya ofisi hizo jambo lililowafanya wananchi kutawanyika kwa hofu.

Alisema Barnad akiwa na viongozi wa Chadema walienda kufungua  taarifa namba Ar/RB/982/2014 kwenye kituo kidogo cha polisi kilicho kona ya Mbauda karibu kabisa na ofisi hizo za CCM ambapo waliwaeleza polisi kuwa mtuhumiwa yuko ndani ya ofisi hizo lakini hawakutaka kwenda kumkamata.

KESI YA KWANZA

Oktoba 2, mwaka jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumfutia kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili.

Lema alishitakiwa kwa kutoa kauli ya uchochezi kuwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alienda kwenye Chuo cha Uhasibu Arusha kama anaenda kwenye sherehe za kuaga mtoto wa kike “send off”.

Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi, Devota Msofe, baada ya wakili wa serikali, Eliananyi Njiro, kutumia kifungu cha 20 kifungu kidogo cha 1 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kuliondoa shauri hilo ambalo lilikuwa lianze kusikilizwa kwa siku mbili mfululizo.

Awali, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mnamo Aprili 24, mwaka jana, Lema akiwa eneo la Freedom Square ndani ya Chuo cha Uhasibu, alitoa maneno ya uchochezi yaliyosababisha uvunjifu wa amani.

Maneno hayo ilidaiwa kuwaq yalitamkwa kinyume cha kifungu cha 390 sura ya 35 cha sheria ya kanuni ya adhabu, marejeo ya mwaka 2002

Kauli hizo zilidaiwa zilipandisha hasira za wanafunzi ambao walianza kumrushia mawe na chupa Mkuu wa Mkoa, Mulongo alipokuwa akiwahutubia kuhusiana na tukio la kifo cha mwanafunzi, Henry Koga kilichotokea Aprili 23, mwaka jana.
Kabla ya kumfungulia mashitaka Lema, Polisi walivamia nyumbani kwake na kumkamata usiku wa manane.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa