MWENYEKITI
wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Fabian Lubuva, amelitaka Jeshi la
Polisi mkoani hapa kutumia busara watakapokuwa wakiimarisha ulinzi
wakati wa zoezi la upigaji kura kwenye Kata ya Sombetini unaotarajiwa
kufanyika kesho ili kuepuka kuwatisha wapiga kura.
Jaji Lubuva aliyasema hayo jana wakati akizungumza na viongozi wa
vyama vya siasa, vinavyoshiriki uchaguzi mdogo kwenye Kata ya Sombetini.
Alisema anatarajia kuzungumza na polisi ili awaombe wachukue
tahadhari wakati wa kulinda na kuimarisha usalama wakati wa kupiga kura.
Awali Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA) wilayani
Arusha, Martin Sarungi, alielezea hofu yake juu ya gari la polisi la
maji ya kuwasha “washawasha” linalozunguka kwenye kata hiyo pamoja na
magari mengi yaliyojaa polisi wenye silaha, kwamba yanaweza kuwatisha
wapiga kura.
“Kama wanasiasa tunatimiza wajibu wetu wa kuhamasisha watu kujitokeza
kupiga kura, lakini tunapata wasiwasi kama lengo linaweza kufikiwa
endapo polisi wataendelea kupita mitaani na magari mengi wakiongozana na
lile la maji ya kuwasha.
“Tunawahofia watu wa umri mkubwa na wakina mama wanaweza kuogopa kwa
kuona pengine kuna vurugu zinaweza kutokea na wao wakashindwa kukimbia,
hivyo wakaamua wasije kabisa kupiga kura,” alisema Sarungi.
Mwenyekiti wa CHADEMA wilayani hapa, Ephata Nanyaro, aliomba NEC
ilielekeze Jeshi la Polisi kukabidhi shahada za wapiga kura wa Kata ya
Sombetini ambazo wanazishikilia kama dhamana badala ya kuzikabidhi kwa
moja ya vyama.
Alielezea wasiwasi wake juu ya kujirudia kwa matukio ya chama ambacho
hakukitaja jina kutumia mabaunsa kutishia watu wanaowahisi hawawaungi
mkono kuwazuia wasiende kupiga kura, hivyo akaiomba NEC izuie matumizi
ya mabaunsa.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapa, Wilfred Ole
Soleili, aliomba tume hiyo kuongeza idadi ya askari polisi na magari ili
kuhakikisha hali ya usalama inakuwepo.
Kaimu Katibu wa Wilaya wa Chama Cha Wananchi (CUF), Mwanaisha,
aliwataka viongozi wa CCM na CHADEMA kuisadia polisi kwa kufuata sheria
ili kuepusha vurugu, huku akitolea mfano wa chama chake alichodai kuwa
wamekuwa wakijitahidi kufunga mikutano yao kabla ya wakati ili kuepusha
vurugu.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia aliyekuwa diwani wa kata hiyo kwa
tiketi ya CCM, Alfonce Mawazo kukihama chama hicho na kujiunga na
CHADEMA.
Majina ya wagombea na vyama vyao kwenye mabano ni Ally Bananga (CHADEMA), David Mollel (CCM) na Ally Mkali, (CUF) .
Kata hiyo ina jumla ya wapiga kura 28,273 ambapo kutakuwa na vituo
vya kupigia kura 62, wasimamizi wa uchaguzi 186 ambapo kila kituo
kitakuwa na msimamizi msaidizi na karani ambapo pia watakuwepo
wasimamizi wasaidizi wa akiba wanne.
0 comments:
Post a Comment