Home » » Wawili wafariki kwa kufukiwa na kifusi

Wawili wafariki kwa kufukiwa na kifusi

Mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo
Watu wawili wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na kifusi katika machimbo ya kokoto katika eneo la Terat, nje kidogo ya Jiji la Arusha.
 
Kufuatia tukio hilo  serikali mkoani Arusha imepiga marufuku uchimbaji wa kokoto katika eneo hilo na kuagiza kamati iliyoundwa mwaka jana baada ya ajali kama hiyo kutokea katika eneo la Moshono kufanya uchunguzi katika migodi yote.
 
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, ametoa amri hiyo baada ya kufika katika eneo la tukio na kuongea na viongozi wa eneo hilo.
 
Kwa mujibu wa Mulongo kamati hiyo itatakiwa kuleta mapendekezo ya namna ya  kuboresha hali ya usalama katika machimbo.
 
“Ile kamati sasa itaanza upya kuchunguza hali ya usalama na kuleta mapendekezo ya kuhakiki hali ya usalama,” alisema Mulongo.
 
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Joseph Solomon  (18) na Saimon Petro (15), wote wakazi wa Muriet.
 
Katika hatua nyingine jeshi la polisi mkoani  Arusha kupitia kwa kamanda Sabas limewataka watu wanaomiliki migodi ya uchumbaji wa kokoto kuhakikisha kuwa wana vibali vya kufanya kazi hiyo.
 
“Tunapiga marufuku haya machimbo yanayoanzishwa kiholela na kuhatarisha maisha ya watu, tutaanza kufuatilia na kuchukua hatua kwa kushirikiana na vyombo vingine vya serikali,” alisema Sabas.
 
Aliongeza kuwa pia katika migogodi hiyo wahakikishe kuwa kuna usalama wa kutosha ikiwemo miundombinu ya tahadhari na uokoaji.
 
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa lilitokea saa 3 asubuhi jana katika machimbo hayo baada ngema kuwaangukia vijana waliokuwa wakichimba na kupakia moram katika gari lililofika katika machimbo hayo.
 
“Lilitokea ghafla sana mimi nilikuwa juu mara nikasiakia ngema inakatika yaani nilishuhudia wenzangu wakifunikwa na udongo na kupoteza maisha,” alisema manusura Loiruk Sandamu.
 
Tukio hilo ni la pili kutokea katika machimbo ya kokoto jijijni Arusha baada ya Machi 16, mwaka jana kuanguka na kufukia watu 16 katika eneo la Moshono.
 
 
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa