WANANCHI 43 wa vijiji vya Kiding’a, Moivo, Kirevi, Sambasha na
Kiranyi, wilayani Arumeru wamesema wapo tayari kupisha ujenzi wa
barabara ya Mianzini hadi Timbolo yenye umbali wa kilomita nane endapo
watalipwa fidia ya mali walizoendeleza pembezoni mwa barabara hiyo
zenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 3.2.
Hayo yalielezwa juzi kwa nyakati tofauti na mashahidi watano wa
upande wa waleta maombi, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha,
Fatma Mssengi, anayesikiliza shauri la ardhi namba 18/2013
lililofunguliwa na wananchi hao.
Wakiongozwa na wakili wao, Modest Akida, mashahidi hao walidai wako
tayari kubomoa nyumba zao na kupisha ujenzi wa barabara hiyo endapo
Halmashauri ya Wilaya ya Arusha ambaye ndiye mdaiwa kwenye shauri hilo
itawalipa fidia stahiki kwa mujibu ya sheria ya barabara ya mwaka 2007.
Shahidi wa tatu, Gideon Lukumay (74), aliieleza mahakama hiyo kuwa
maeneo hayo wanayamiliki kwa mujibu wa sheria za kimila, kwani
waliyarithi kutoka kwa mababu.
Alidai anachojua barabara hiyo ni mali ya wananchi, kwani ndiyo
wamekuwa wakiikarabati kwa kipindi chote kabla Halmashauri ya Wilaya ya
Arusha kuanza kuikarabati.
“Baada ya nyumba zetu kupigwa alama ya ‘X’ tulipeleka malalamiko
halmashauri na kuiuliza kwanini inataka kutubomolea bila kufidiwa
lakini hatukupata majibu yanayoeleweka, binafsi ningefidiwa
ningeondoka,” alidai Lukumay.
Shahidi wa kwanza, Fanuel Lamai, alieleza kuwa Aprili 14, mwaka jana
halmashauri walitumia katapila na kuvunja kingo za barabara, kukata
miti kwa kutumia mashine huku zoezi hilo likifanyika chini ya uangalizi
wa polisi.
Alielea kuwa hawapingi ujenzi wa barabara hiyo ila wanaomba kulipwa fidia.
Upande wa waleta maombi wamemaliza kutoa ushahidi wao ambapo walileta
mashahidi watano, wakiwemo Agnes Martin (67) na Ndeai Nembate.
Katika madai yao ya msingi wananchi hao 43 wanaiomba mahakama hiyo
itamke kuwa wao ni wamiliki halali wa ardhi na mali zao zilizopo maeneo
ya pembezoni mwa barabara ya Mianzini mpaka Timbolo.
Pia wanaiomba mahakama hiyo iwaelekeze Halmashauri ya Wilaya ya
Arusha iwalipe fidia ya ardhi waliyoiendeleza na mali zao yenye thamani
ya zaidi ya sh bilioni 3.2, ili waweze kupisha ujenzi wa barabara hiyo
ya Mianzini mpaka Timbolo.
Chanzo:Tanzania Dima
0 comments:
Post a Comment