WAKATI
wimbi la ujangili wa meno ya tembo na pembe za faru likizidi kushika
kasi nchini, Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya WMA Enduimet iliyopo
Wilaya ya Longido, mkoani Arusha imefanikiwa kuzuia ujangili wa tembo
kwa miaka mitatu mfululizo.
Tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo hadi sasa hakuna tukio la ujangili
wa tembo wala faru lililoripotiwa kutokana na jamii hiyo kuhamasika juu
ya masuala ya uhifadhi, sanjari na kila mwanakijiji wa eneo hilo kuiona
hifadhi hiyo kama sehemu ya ustawi wa maisha yake.
Ofisa tawala wa jumuiya hiyo, William Kuyan, alisema kinachowasaidia
ni namna walivyojizatiti kwa kila mwanakijiji, katika kuzuia aina yoyote
ya ujangili ndani ya hifadhi husika.
“Sio kwamba hakuna majangili, wapo wengi, tunawakamata kila siku
kwenye doria zetu na tunawafikisha kwenye vyombo vya sheria,” alisema.
Akizungumza wakati wa doria ya kusaka majangili ndani ya hifadhi
hiyo, Kamanda wa Kikosi cha Operesheni cha askari wa Hifadhi ya Jamii
WMA Enduimet, John Magembe, alisema suala la uhifadhi wa wanyamapori
linawezekana kama kila mwananchi atakubali, kujitolea na kuwa mwaminifu
kwa uhifadhi huo na matokeo ya rasilimali zake.
Alisema siri ya mafanikio yao ni namna wanavyoshirikisha wanavijiji
wenzao katika kuwezesha kupata taarifa za kila mgeni anayeingia kijijini
hapo, lakini pia hufanya doria za miguu, mbwa wa kunusa, kutumia ndege
maarufu kama ‘popobawa’ na zaidi hutumia watoa taarifa.
Kamanda wa Kikosi cha Mbwa, Lembris Kephas, alisema mbwa hao wana
uwezo wa kumtambua jangili au yeyote aliyepita na kukanyaga ndani ya
hifadhi kwa kutumia pua zao.
“Wakati wa doria tukigundua kuna nyayo za mtu amepita ndani ya
hifadhi humsogeza mbwa huyo kwa ajili ya kunusa nyayo hiyo, na huyu mbwa
ana uwezo wa kuhifadhi harufu hiyo kwa muda wa siku saba,” alisema
Kephas.
Aliongeza kwa kusema baadaye wanapowashuku watuhumiwa au
wanapowakamata majangili wakati wa gwaride la utambuzi, mbwa hao hupita
kwenye miguu ya watuhumiwa hao na anapobaini uwiano wa harufu hupiga
magoti au kukaa chini ya miguu ya mtuhumiwa kuashiria ndiye aliyekatisha
kwenye hifadhi.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment