Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kwamba hakuna tume itakayoundwa kuchunguza tukio la ulipuaji wa bomu hilo katika mkutano wa Chadema wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi wa udiwani jijini humo katika viwanja vya Soweto.
“Napenda kuliarifu Bunge kwamba hakuna tume itakayoundwa kuchunguza tukio hilo, tunavyo vyombo vya dola vinavyoheshimika kufanya kazi hiyo…wale wenye ushahidi wanaweza kuwasilisha, watupe ushirikiano badala ya kukimbia na ushahidi kwenye brief-case,” alisema Dk. Nchimbi.
Alisema wizara yake imewasiliana na Rais Jakaya Kikwete ambaye amekubali kuanzisha kitengo cha intelijensia katika masuala ya uhalifu, ili kudhibiti uhalifu na kufuatilia matukio kama hayo.
Waziri Nchimbi alikuwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge na pendekezo la kuunda tume kuchunguza tukio la mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa Chadema eneo la Soweto lililotolewa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) ambaye aliikumbusha serikali haja ya kuunda tume hiyo ili chama chao kipeleke ushahidi wa mtu aliyelipua bomu hilo.
Katika mlipuko huo uliotokea Juni 14, mwaka huu, watu watatu walifariki na wengine kudhaa kujeruhiwa.
Mlipukohuo ulitokea wakati Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyekuwa akimalizia hotuba yake ya kufunga kampeni za chama chake na huku wanachama wakijiandaa kufanya harambee.
Mkutano wa Chadema ulikuwa wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani kwa kata za Themi, Elerai, Kaloleni na Kimandolu. Chadema ilishinda kata zote.
Tukio hilo liliacha maswali mengi kutokana na vyombo vya dola kushindwa kumtia mbaroni hata mtuhumiwa mmoja na kumfungulia mashitaka.
Kikubwa ambacho kimekuwa kikiibua maswali ni madai kuwa mtu mmoja ambaye hajafahamika ndiye aliyerusha bomu hilo kwenye mkusanyiko wa watu waliohudhuria mkutano huo.
Kufuatia mlipuko huo, polisi waliokuwa wakifanya ulinzi katika mkutano huo, walilipua risasi za moto na inadaiwa kuwa zaidi ya watu 6O hadi 70 walijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Selian inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati na wengine walilazwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Tangu kutokea kwa mlipuko huo hakuna taarifa zozote zilizotolewa na vyombo vya dola kuhusu maendeleo ya uchunguzi, na kwa upande mwingine Chadema imekuwa ikiishinikiza serikali kuunda tume huru ya uchunguzi ili kiwasilishe ushahidi ilionao wa mtu aliyehusika katika mlipuko huo.
Mbali na kuishinikiza serikali kuunda tume huru kuchunguza tukio hilo, viongozi kadhaa wa Chadema wamekuwa wakidai kuwa mmoja wa askari Polisi ndiye aliyehusika kurusha bomu hilo.
Tukio lingine ambalo liliacha mashaka kutokana na vyombo vya dola kushindwa hadi sasa kuwakamata na kuwafungulia mashitaka watuhumiwa ni la mlipuko wa bomu wa Mei 5, mwaka huu lililosababisha vifo vya takribani watu wanne na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa katika Kanisa Katoliki la Olasiti nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Watu hao walifariki na kujeruhiwa wakati wa ibada maalum ya kuzindua kanisa la parokia mpya ya mtakatifu Yosefu iliyohudhuriwa pia na Balozi wa Papa nchini pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Askofu Mkuu Josephat Lebulu.
Jeshi la Polisi pia limekuwa likilaumiwa kwa kusuasua kutoa taarifa za kuwakamata wahusika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria kutokana na tukio hilo kuchukua muda mrefu.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment