Arusha
Home » » KIKAO CHA 24 CHA BODI YA TAIFA YA PAROLE CHAANZA LEO JIJINI ARUSHA

KIKAO CHA 24 CHA BODI YA TAIFA YA PAROLE CHAANZA LEO JIJINI ARUSHA

Kikao cha 24 cha Bodi ya Taifa ya Parole kimeanza leo Desemba 19, 2013 chini ya
Uenyekiti wa Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo katika Ukumbi wa Hoteli ya Charity
iliyopo Jijini Arusha.

Kikao hiki cha siku mbili kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Sekretarieti ya Bodi
ya Taifa ya Parole kitajadili Wafungwa waliopendekezwa kuachiliwa kwa Parole. Aidha,
Wajumbe watapitia mapendekezo ya Maboresho ya Sheria ya Bodi za Parole(Cape 400 RE
2002) pamoja na kuchambua maoni yanayohusu taarifa ya Mhe. Jaji Kiongozi ya kusamehe
theluthi moja (1/3 ) ya Kifungo kwa washitakiwa watakaokiri Mahakamani.

Utaratibu huu wa Parole hapa nchini ni moja wapo ya adhabu mbadala wa kifungo ambao
ni matokeo ya mfumo uliobuniwa na jamii katika nchi nyingi kwa miaka ya hivi
karibuni ikiwa ni njia moja wapo ya kupunguza ongezeko la wafungwa ndani ya Magereza
hivyo kuipunguzia Serikali na Wananchi ambao ndio walipa Kodi, Mzigo mkubwa wa
kuwahudumia Wafungwa wawapo ndani ya Magereza.

Lengo Kuu la Sheria ya Bodi ya Parole ya Mwaka 1994 ambayo ilifanyiwa marekebisho
Mwaka 2002 ni kuweka masharti Maalum kuhusu utaratibu wa Urekebishaji wa Wahalifu
nje ya Magereza baada ya Mfungwa kutumikia sehemu ya kifungo chake na kuonesha
mwelekeo wa kurekebika unaokubalika kwa mujibu wa Sheria hii na Kanuni zake.

Kumekuwepo  changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Sheria hii ikiwa ni pamoja
na ufinyu 
au wigo mdogo wa Kisheria uliowekwa na Sheria yenyewe. Kutokana na wigo mdogo uliopo
wa Kisheria takwimu zilizopo zinaonesha kuwa wafungwa wengi hawawezi kujadiliwa kwa
kuwa hawana sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa Sheria iliyopo.

Kwa mujibu wa Sheria hiyo Mfungwa anayestahili Parole ni yule anayetumikia kifungo
cha miaka minne(4) na kuendelea na awe ametumikia theluthi moja (1/3) ya kifungo
chake na kuonesha mwelekeo wa kurekebika unaokubalika kwa mujibu wa Sheria hii na
Kanuni zake.

Hiki ni Kikao cha Tatu kufanyika chini ya Uenyekiti wa Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia
Munuo tangu ateuliwe na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole Aprili, 2013.
Sources:Insp. Lucas Mboje, Arusha 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa