Arusha
Home » » Wanaharakati wataka siasa iepukwe vita dhidi ya ujangili

Wanaharakati wataka siasa iepukwe vita dhidi ya ujangili

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki
Wanaharakati  wa Tanzania waliotembea siku 19 kutoka Arusha hadi Dar es Salaam kupinga ujangili wa tembo, wamepongeza hatua zilizoanza kuchukuliwa na wananchi na vyombo mbalimbali vya serikali, kufanikisha kukamatwa kwa raia watatu wa China na vipande 700  vya meno ya tembo.
Wanaharakati hao, Mkazeni Yakobo na Kaptorina Maryange waliotembea umbali wa zaidi ya kilometa 600 kutoka Arusha hadi jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 24 hadi Septemba 12 mwaka huu, wameeleza kufarijika na hatua zilizoanza kuchukuliwa na wadau mbalimbali kuwafichua majangili wa tembo.

Walitoa wito kwa wananchi kuendelea na uzalendo wa aina hiyo kwa kuwafichua wahujumu zaidi na kulinda rasilimali na maliasili zote ambazo ni tunu na faida kwa taifa, na kutaka siasa iwekwe pembeni katika maamuzi dhidi ya watuhumiwa wa ujangili na badala yake sheria iachwe ichukue mkondo wake.

Walitoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kufichua taarifa za majangili wanaokamatwa na hata wanaokusudia kufanya ujangili, ili kusaidia kukomesha vitendo hivyo, kwani nafasi yao ni kubwa katika kuwafahamisha wananchi kinachoendelea.

Wiki iliyopita, raia wawili wa China walikamatwa katika eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam wakiwa na vipande 706 vya meno ya tembo, huku wananchi wa eneo hilo wakidai wanachofahamu ni kuwa raia hao wamekuwa wakijushughulisha na biashara ya ndimu na vitunguu na hawakujua siri nyingine iliyokuwa nyuma ya pazia ya biashara haramu ya meno ya tembo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki alisema vipande hivyo vinakadiriwa kuwa sawa na zaidi ya tembo 200 waliouawa.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa