WANAHARAKATI wa haki za binadamu wanakusudia
kumchukulia hatua za kisheria ikiwamo kumfikisha mahakamani, Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kutokana na agizo lake la kutaka
watu watakaokamatwa kwa ujangili kuuawa.
Hatua ya kumburuta mahakamani Waziri Kagasheki
inakuja wakati wanaharakati hao wakiwa wamemfungulia mashitaka Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, kutokana na kauli yake ya kulitaka Jeshi la Polisi kuwatandika
watu watakaokaidi amri ya polisi.
Katika mashambulizi hayo, wanaharakati hao
wamemtaka ajiuzulu uwaziri kwa madai kuwa kauli yake imetia aibu kwa
serikali na haikupaswa kutolewa na kiongozi wa juu kama yeye.
Hayo yalisemwa jana kwa nyakati tofauti na
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi isiyo ya kiserikali ya kutetea wafugaji (PINGO’s),
Edward Porokwa, na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu,
(LHRC), Hellen Kijo-Bisimba.
Bisimba alisema kuwa mwendelezo wa kauli
zinazovunja sheria za nchi zinazotolewa na viongozi ikiwemo ile ya Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda ya kutaka wasiotii maagizo ya Jeshi la Polisi wapigwe zitafanya
nchi ishindwe kutawalika.
Alisema kuwa ni aibu kwa mtu mwenye wadhifa wa
waziri kutoa kauli ya kutaka watuhumiwa wa ujangili wauawe kwa kile alichoeleza
kuwa si kila anayekutwa kwenye hifadhi ni jangili.
Alisema kuwa kuna wengine wanaingia kuchunga mifugo
au kukamata wanyama wadogo kwa ajili ya kitoweo, hivyo ni vema wakapelekwa
kwenye vyombo vya sheria ili waweze kuthibitika kama ni majangili au la na si
kuwaua.
Bisimba alisema kuwa kama Waziri Kagasheki anaona
sheria za nchi zina matatizo ni vema akapeleka marekebisho ya sheria bungeni
lakini si kutoa kauli za kuifanya nchi isifuate utawala wa sheria huku
akisisitiza kuwa kauli hiyo ni aibu kubwa kwa taifa.
Alisema kuwa kwa sasa wanajipanga ili kujua ni
hatua gani za kuchukua kutokana na kauli hiyo ya Waziri Kagasheki aliyedai kuwa
kwa nafasi yake angeweza kuviongezea uwezo vyombo vya ulinzi na usalama
vinavyokabiliana na ujangili kwa kuvipa vifaa na teknolojia za kisasa za
kukabiliana na majangili lakini si kuamrisha kuua watu.
Alisema kuwa kauli kama hiyo iliwahi kutolewa miaka
kati ya 1996 na 1997 na aliyekuwa Waziri wa Maliasili, Juma Ngasongwa, ambapo
ilisababisha watu tisa waliokuwa wanaishi kuzunguka Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti kupangwa mstari na kupigwa risasi wakidaiwa kuwa ni majangili,
jambo ambalo halikuwa kweli.
Bisimba alisema kuwa kati ya wale watu
tisa, wawili hawakufa ndiyo wakatoa taarifa kwao, ambapo suala hilo
walilipeleka mbele ya Tume ya Haki za Binadamu.
Hata hivyo aliweka wazi kuwa hakubaliani na vitendo
vya ujangili vinavyoendeshwa na kuhatarisha uwepo wa tembo lakini akasema kuwa
yeye anataka sheria za nchi zilifuatwe kwa majangili hao kukamatwa na
kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na si kuuawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Pingo’s, Porokwa,
alisema kuwa ni vema Waziri Kagasheki akajiuzulu na aombe radhi kwa kauli yake
ya kuchochea wananchi na vyombo vya usalama kuua watu.
“Hatupendi ujangili ila hili la waziri kuagiza watu
wajichukulie sheria mkononi halikubaliki ni vema akajiuzulu, anaudharau muhimili
wa mahakama kwa kigezo cha faini ndogo? Hii haikubaliki, yaani waziri aamue
kutangaza watu wauawe?
“Mwenye mamlaka ya kutangaza hali ya hatari ni Rais
ambaye ni amiri jeshi mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama lakini pia hana haki
ya kusema watu wauawe hovyo tu,” alisema Porokwa.
Alisema kwa kuwa Kagasheki kajipambanua wazi kuwa
yeye si mtetezi wa haki za binadamu pale alipowataka watetezi wa haki za
binadamu wafunge midomo, hivyo ni vema akajiuzulu wadhifa alio nao ili nafasi
hiyo ichukuliwe na mtu mwenye kusimamia na kuheshimu haki za binadamu ambaye
atakuwa muumini wa utawala wa sheria .
Porokwa alisema kuwa kauli hiyo ya Kagasheki
itasababisha mauaji kwa wananchi wasio na hatia wanaoishi kuzunguka hifadhi za
taifa na kwamba kuna matukio ya wananchi wanaochunga mifugo pembezoni mwa
hifadhi hizo kukamatwa na walinzi wa hifadhi na kusingiziwa kuwa wameingiza
mifugo hivyo kulipishwa faini.
Alisema kwa kauli ya waziri wananchi hao watauawa
wakidaiwa ni majangili, jambo alilodai kuwa ni hatari, ingawa alikiri
kutokubaliana na ujangili unaohatarisha kutoweka kwa tembo.
Porokwa alisema kuwa ni vema wale watakaokamatwa
wakifanya ujangili wakapewa haki ya kusikilizwa kwa kufikishwa kwenye vyombo
vya sheria, ambavyo vina uwezo wa kuwahukumu kama wakithibitika ni majangili na
si kuwaua.
Mwishoni mwa wiki Waziri Kagasheki akiwa jijini
Arusha akiongea mara baada ya kuongoza matembezi ya kupinga mauaji ya tembo
aliwataka wale watakaokutana na majangili kumalizana nao huko huko.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment