MATUKIO ya kumwagiwa tindikali yanazidi kushika
kasi ambapo mfanyabiashara, Japhet Minja (30) mkazi wa Sakina, amemwagiwa kitu
kinachodhaniwa kuwa ni tindikali usoni na watu wasiojulikana.
Tukio hilo lilitokea juzi saa tatu asubuhi maeneo
ya Shamsi ambako mfanyabiashara huyo anapatiwa matibabu kwenye hospitali ya
Selian huku macho yake yakiwa yamepoteza uwezo wa kuona.
Akizungumza kwa tabu, Minja ambaye alitolewa kwenye
chumba cha uangalizi maalumu (ICU) jana mchana, alisema kuwa anasikia maumivu
makali kwenye macho na ngozi ya uso.
Alisema kuwa Oktoba 8 mwaka huu, wakati akitoka
nyumbani kwake maeneo ya Sakina Banda la Maziwa alisimamishwa kwa kupigiwa honi
na watu waliokuwa kwenye gari dogo aina ya Vitz ambayo hakumbuki namba zake za
usajili.
Minja alisema kuwa alisimama na kuwasikiliza watu
wawili waliokuwa kwenye gari hilo ambao walimweleza kuwa walikuwa wanampigia
simu kwa namba alizobandika ubavuni mwa gari lake, lakini hawampati, wanahitaji
kuwekewa madirisha ya aluminum kwenye nyumba yao na walimpa vipimo.
Alisema kuwa aliwaambia ni vema akafika kwenye eneo
husika, lakini walimsisitiza atumie vipimo walivyokuwa navyo, na aliwapigia
mahesabu ikaonekana inahitajila zaidi ya sh milioni 4.4.
Kwa mujibu wa Minja, wateja hao walimpa kiasi cha
sh milioni tatu kama malipo ya awali, kiasi kingine wangempa akimaliza kazi na
kwamba alitaka kuzihesabu fedha hizo, lakini wakamwambia hazina shida
akahesabie ofisini kwake, hivyo alizihifadhi ndani ya gari.
“Tuliondoka tukiwa tumeongozana, kufika mbele
kidogo tukakuta gari nyingine aina ya Vitz likiwa liimeegeshwa
kuziba barabara, ndani kulikuwa na watu wanne.
“Nikaona wale watu wawili walionipa fedha wameenda
kuzungumza nao, lakini hawakuondoa gari, hivyo na mimi nikasogea na kuwaomba
waondoe gari kwani wengine tunawahi kazi,” alisema.
Alisema kuwa watu wale walishuka na kuanza kumpiga
kisha mmoja akampulizia kitu kwenye macho, yakaanza kutoa machozi huku wale
waliompa fedha wakikimbilia ndani ya gari lake na kuzichukua.
“Niliamua kukimbilia kwenye gari langu na kurudi
nyuma kwani bado yale magari yalikuwa yameziba njia. Nilikwenda duka la dawa
wakanimwagia maji usoni na spiriti kwenye kidonda cha mkononi nilipong’atwa
kisha wakanishauri niende hospitali.
“Niliendesha gari hadi hospitali ya Selian na
wakati wakienda kunipatia huduma nilihisi kushindwa kupumua na nikapoteza
fahamu na nilipozinduka baadaye nikajikuta ICU,” alisema.
Dk. Godbless Massawe aliyempokea Minja, alikiri
kuwa alimwagiwa kitu ambacho hadi sasa hawajaweza kukibaini kwani vipimo vya
kubaini tindikali kwa hapa nchini vinapatikana kwenye Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili pekee.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment