Mwenyekiti
wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amepinga uamuzi wa kusimamishwa kwa
maelezo kuwa kikao kilichochukua uamuzi huo hakitambuliki kikatiba huku
akikanusha tuhuma za kutumiwa na Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe,
kukisambaratisha chama hicho.
Akizungumza
jana na gazeti hili, Mwigamba alisema kikao ambacho kina mamlaka ya
kumwajibisha ni Kamati Kuu baada ya kupokea tuhuma na kumsikiliza.
“Baraza
la uongozi la Kanda halina mamlaka ya kunisimamisha uenyekiti, lakini kwa kuwa
mimi bado ni mwanachama hai wa Chadema na sitahama Chadema, nitakaa pembeni ili
chama kifanye uchunguzi wa tuhuma zangu nikiwa nje ya ofisi,” alisema Mwigamba.
Hata
hivyo, alisema anakusudia kufafanua chanzo cha mgogoro wake na baadhi ya
viongozi leo, baada ya kukabidhiwa kompyuta mpakato (laptop) na viongozi wa
chama hicho ambao waliichukua ili kuifanyia uchunguzi.
Akana
kutumiwa na Zitto
Akizungumzia
tuhuma za muda mrefu kuwa, amekuwa akitumiwa na Zitto hasa kuelekea uchaguzi
ndani ya chama hicho, alisema wanaofikiri hivyo ni vipofu wa kisiasa.
“Hizi
tuhuma kuwa natumiwa na Zitto nimekuwa nikizisikia, lakini huo ni upofu, mimi
si mtu wa kutumika nina elimu yangu nzuri ya shahada ya kwanza ya utawala wa
biashara, najua ninachokifanya ni kwa masilahi ya chama,” alisema Mwigamba.
Alisema
kama angekuwa mtu wa kutumiwa sasa, angetumiwa na mwenyekiti wa chama hicho,
Freeman Mbowe ambaye ana uwezo wa kifedha kuliko Zitto au Katibu Mkuu, Dk
Willibrod Slaa ambaye atakuwa mgombea wa urais wa chama hicho na ana uwezekano
wa kushinda.
Alisema
kabla ya tuhuma za sasa kwamba anatumiwa na Zitto, aliwahi kutuhumiwa pia na
Zitto kuwa anatuhumiwa na Mbowe hasa kutokana na misimamo yake na kauli zake
katika vikao na maeneo mbalimbali, lakini baadaye ilithibitika kuwa alikuwa na
hoja za msingi.
“Mimi ni
mwanachama hai wa Chadema na nimekuwa nikitoa maoni yangu si kama Mwenyekiti wa
Chadema Mkoa. Nina uhuru wa kutoa maoni katika kuhakikisha chama changu
kinashika dola,” alisema Mwigamba.
Mwenyekiti
wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Mchungaji Israel Natse alitangaza juzi
kusimamishwa Mwigamba hasa kutokana na tuhuma za kukichafua chama hicho kwenye
mitandao ya kijamii.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment