MTALII mmoja raia wa Marekani, Thomas Macfee (58),
ameuawa na kundi la tembo wakati akiwa kwenye kambi ya Kakoi Tarangire eneo
linalodaiwa kuwa ni mapito ya asili ya wanyama hao.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Musa Marambo,
alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 30 mwaka huu, saa 2:30 asubuhi baada
ya mtalii huyo akiwa na wenzake watano ambao majina yao hayakupatikana kujaribu
kupiga picha za kundi kubwa la tembo lililokuwa likipita karibu na eneo
walilokuwa.
Alisema kuwa wakiwa kwenye harakati za kupiga
picha, ghafla tembo hao walibadili uelekeo na kuanza kuwafuata ndipo wakaanza
kukimbia ambapo kwa bahati mbaya Macfee alinasa kwenye dimbwi la matope.
“Baada ya kunasa kwenye matope alishindwa kutoka
ndipo tembo wale wakaanza kumpitia juu na baada ya hapo wenzake walienda
kumchukua na kumuwahisha kwenye zahanati ya hifadhi ya taifa ya Tarangire ndipo
akafariki,” alisema Manyara.
Alisema kuwa baada ya kufariki alipelekwa
kuhifadhiwa kwenye hospitali ya Selian jijini Arusha ambapo ubalozi wa Marekani
ulimchukua kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Meneja uhusiano wa Tanapa, Paschal Shelutete,
alitoa taarifa kwa vyombo mbalimbali vya habari akifafanua kuwa eneo alilokuwa
mgeni huyo ni nje ya hifadhi yao.
“Tukio la mgeni husika lilitokea nje ya hifadhi ya
Tarangire katika kijiji cha Kakoi kambi ya Tarangire River Camp, wakiwa
wanafanya utalii wa kutembea kwa miguu.”
“Baada ya kuvamiwa na kuumizwa, mgeni huyu
alifikishwa katika zahanati ya Tarangire na watumishi wa kambi aliyofikia
ambayo iko nje ya hifadhi kwa ajili ya matibabu ya huduma ya kwanza ambapo
alifariki,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment