Arusha
Home » » BALOZI IDDI AFUNGUA MKUTANO WA 31 WA KIMATAIFA WA TATHMINI YA ELIMU YA AFRIKA JIJINI ARUSHA

BALOZI IDDI AFUNGUA MKUTANO WA 31 WA KIMATAIFA WA TATHMINI YA ELIMU YA AFRIKA JIJINI ARUSHA


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa 31 ya Kimataifa wa Tathmini ya Elimu ya Afrika unaofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto Mkoani Arusha.
 Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa 31 wa Kimataifa wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mkutano huo iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye hoteli ya Ngurdoto Mkoani Arusha. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
***************************************
Na Othman Khamis Ame
Mataifa ya Bara la Afrika yana wajibu wa kuhakikisha kwamba Elimu inayotolewa na kufundishwa katika Taasisi zote za Elimu Barani humu inakuwa bora na kumnufaisha vilivyo Mtoto wa Afrika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiufungua Mkutano wa 31 wa siku Tano wa Kimataifa wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika { AEAA } unaofanyika katika Ukumbi wa Victoria wa Hoteli ya Ngurdoto iliyopo Mkoani Arusha Tanzania.
Balozi Seif aliwaambia washiriki wa Mkutano huo kutoka Nchi 28 Barani Afrika sambamba na wadau wa Elimu wa Nchi washirika Duniani kwamba Serikali za mataifa hayo wanachama ziangalie njia muwafaka katika kuona hadhi na ubora wa elimu inaendelea kupatikana kwenye mataifa yao.
Alisema mara nyingi wananchi na hasa wazazi wa wanafunzi wamekuwa wakilalamikia kushuka kwa kiwango cha elimu suala ambalo linafaa kuchukuliwa hatua za ziada katika kupatikana kwa vifaa ambavyo ndivyo vinavyochangia kupunguza ubora wa elimu. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPO CHINI
Alisema hivi sasa kiwango cha elimu kinaonekana kuchuka kinachochangiwa na ukosefu wa vifaa vya sayansi jambo ambalo linahitaji mazingatio makubwa katika mabadiliko ya viwango bora vya elimu.
Balozi Seif alieleza kuwa Mkutano huo wa Tathmini ya Elimu ya Afrika umekuja muda muwafaka kwa wanachama hao katika kubadilisha uzoefu wa tathmini ya elimu ambapo utasaidia kujenga nguvu za pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu Barani Afrika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba elimu ndio uti wa mgongo wa maendeleo popote pale duniani, hivyo jitihada za ziada zinapaswa kuchukuliwa katika kuona eneo hilo linajengewa mazingira mazuri na ya uhakika.
“ Na matumaini makubwa kwenu washiriki wa Mkutano huu wa Tathmini ya Elimu ya Afrika kwamba mtatumia fursa na nafasi ya mkutano huu kuondoka na wazo litakalosaidia kuimarika kwa ubora wa elimu Barani Afrika ”. Alifafanua Balozi Seif.
Aliwakumbusha wajumbe wa Mkutano huo kuelewa kwamba Mataifa ya Afrika yamejikubalisha kuimarisha Mpango wa Elimu kwa wote na Malengo ya Milenia hadi ifikapo mwaka 2015 ikiwa ni hatua inaozitaka nchi hizo kufikia.
Hata hivyo Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa kukabiliana na tatizo la kuvuja kwa mitihani ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likichangia kushuka kwa kiwango cha elimu katika mataifa mengi dunia likiwemo Bara la Afrika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitolea mfano wa mpango wa uimarishaji wa elimu unaofuatwa Zanzibar unaofuatwa kuanzia Maandalizi,Msingi, Sekondari hadi chuo Vyuo Vikuu unaweza kusaidia katika baadhi ya Mataifa ya Afrika endapo utafanyiwa utafiti na Jumuiya hiyo ya Tathmini ya Elimu ya Afrika.
Mapema Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika     { AEAA } Dr. Joyce Lazaro Ndalichako alisema lengo la Mkutano huo ni kuangalia njia bora za kuimarisha hadhi ya Elimu katika Mataifa wanachama wa { AEAA }.
Dr. Joyce alisema kwamba Jumuiya yake imekuwa ikitumia njia kadhaa ikiwemo kuwashirikisha wataalamu sambamba na Kamati za Utafiti ili kuhakikisha lengo hilo linafikiwa vyema.
Alisema upo utaratibu wa kubadilishana vipindi na uzoefu katika utunzi wa mitihani kwa hatua ya kujenga nguvu za pamoja za kuimarisha kiwango cha elimu Barani Afrika.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano huo Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Phillip Mulugo alisema wakati umefika kwa Taasisi za elimu kuhakikisha ongezeko la Maskuli popote pale linakwenda sambamba na ubora wa elimu.
Mh. Mulugo alifahamisha kwamba mfumo huo ukitekelezwa kwa pamoja unaweza kusaidia kupata wataalamu wenye kiwango kinachokubalika vyema kitaifa na Kimataifa.
Mkutano huo wa 31 wa Kimataifa wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika uliojumuisha washiriki wa Mataifa 28 ya Bara la Afrika umehudhuriwa pia na wadau wa Elimu kutoka mataifa zaidi ya kumi Duniani zikiwemo Uingereza,Marekani, India, China na Ujerumani.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa