- Nassari anadaiwa kumshambulia Husein Warsama, Julai 16 mwaka huu, huko Makuyuni mkoani Arusha
Arusha.. Jeshi la Polisi mkoani Arusha, jana
lilimshikilia Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari
akituhumiwa kumshambulia kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein
Warsama wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Makuyuni, wilayani
Monduli.
Nassari aliyefika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha
saa 2:30 asubuhi jana, alishikiliwa kwa saa tatu na nusu baada ya
kuhojiwa, ambapo aliachiwa saa 6:02 mchana, baada ya kujidhamini
mwenyewe.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Mkuu wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha (RCO) Diwan Nyanda, Nassari
anadaiwa kumshambulia Warsama, Julai 16 mwaka huu, huko Makuyuni
alipokuwa wakala mkuu wa mgombea udiwani kupitia Chadema, Japheth
Sironga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas
hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu zake zote mbili
za kiganjani kuita bila kujibiwa, huku Nyanda ambaye Nassari aliripoti
kwake akikataa kuzungumzia suala hilo na kutaka atafutwe RPC kwa maelezo
kwamba ndiye msemaji wa polisi mkoa.
“Niko njiani naenda Dodoma, mtafute afande RPC, ndiye msemaji wa polisi mkoa,” alisema RCO Nyanda kwa njia ya simu jana.
Hata hivyo, habari za uhakika kutoka duru za
polisi zinaeleza kuwa Jeshi la Polisi alianza kumsaka Nassari tangu
Jumanne iliyopita kupitia kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru.
Habari hizo zilizothibitishwa na Nassari mwenyewe
zimeeleza kuwa Jumatano ya Julai 24 mwaka huu, Naibu Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi, Kamishna Isaya Mngulu alimpigia simu
mbunge huyo kumtaka afike polisi, ndipo walipokubaliana kuwa aende
jana.
Tuhuma zinazomkabili
“Nilipofika polisi na kuripoti kwa RCO, nikawekwa
chini ya ulinzi na kutakiwa kutoa maelezo kuhusu madai ya kumshambulia
mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Husein Warsama siku ya uchaguzi
mdogo wa udiwani Kata ya Makuyuni,” alisema Nassari
Mbunge huyo alisema kuwa baada ya kuwekwa chini ya
ulinzi, RCO Nyanda alimkabidhi kwa ofisa mwingine wa polisi kwa ajili
ya mahojiano, lakini alikataa kuandikisha maelezo yoyote kwa sababu
hakuwa ameambatana na wakili wake.
Nassari alifafanua kuwa maelezo hayo yalionekana
kuwaudhi polisi ndipo RCO aliagiza awekwe mahabusu hadi wakili wake,
Tundu Lissu na Mabere Marando watakapofika, huku polisi kutoka wilayani
Monduli wakiwa wamefika tayari kumchukua na kumpeleka huko kutokana
tuhuma zinazomkabili kuwa zilifanyikia wilayani humo.
“Baada ya mimi kuwa tayari kuwekwa mahabusu na
kuanza kukabidhi vifaa vyangu, RCO na maofisa wengine wa polisi
waliokuwepo, walifanya majadiliano mafupi na baadaye kunikubalia
kujidhamini mwenyewe, huku polisi wakiahidi kunipigia simu wakati wowote
nitakapohitajika,” alisema Nassari
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment