Arusha
Home » » Kesi ya Lema Uhasibu yaiva

Kesi ya Lema Uhasibu yaiva

UPANDE wa Serikali katika kesi inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema, Godbless Lema ya kudaiwa kumtukana Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mullongo umeiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwamba utawasilisha mashahidi tisa. Hatua hiyo inatokana na Lema kukana mashitaka aliposomewa maelezo ya awali.
Kesi hiyo itaanza kusikilizwa mfululizo Agosti 20, 21 hadi 22 mwaka huu.

Akisoma maelezo ya awali jana,Wakili wa Serikali Eliainenyi Njiro alidai Lema akiwa katika eneo la Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) April 24, mwaka huu alitoa maneno ya kashfa kwa Mulongo.

Lema alisomewa shitaka jingine la uvunjifu wa amani akiwa katika chuo hicho.

Njiro alinukuu maneno yanayodaiwa kutamkwa na Lema akiwa katika eneo la chuo kuwa ni pamoja na, "Mkuu wa Mkoa anakuja hapa kama anaelekea kwenye send off na hajui mahali chuo hicho kilipo… Mkuu wa Mkoa ameshindwa kuwapa pole wanafunzi baada ya kufiwa na mwanafunzi mwenzao.

"Mkuu wa Mkoa hawezi kuzungumza na wanafunzi wasio na nidhamu ingawa hakuwasaidia kutokana na matatizo yao."

Lema kupitia kwa Wakili wake, Method Kimomogolo alikana mashitaka yote.

"Mashitaka ya kumtukana Mkuu wa Mkoa na uvunjifu wa amani katika eneo la chuo mteja wangu hakubaliani nayo," alisema Wakili Kimomogolo.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Hakimu Mkazi Devotha Msofe alikubaliana na pande zote mbili muda wa kuanza kusikiliza ushahidi wa kesi hiyo.
CHANZO GAZETI LA MTANZANIA

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa