na Ramadhani Siwayombe, Arusha
SEREKALI imesema hadi kufikia mwaka
2015 kila Mtanzania atakuwa na anuani ya posta ya makazi kupitia mpango maalumu
unaoendelea wa kuandika namba za nyumba na mitaa kote nchini.
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib
Bilal, alibainisha hayo jana wakati akifungua mkutano wa 32 wa mwaka wa
muungano wa mashirika ya posta Afrika (PAPU).
Alisema mpango huo unaendana
sambamba na dira ya taifa ya mwaka 2015 ambayo imeanisha vipaumbele mbalimbali
ikiwamo hiyo ya kuwapatia wananchi anuani zitakazowarahisishia kufikiwa na
huduma mbalimbali za maendeleo.
Alisema kuwapo na anuani za uhakika
kwa wananchi ni sehemu mojawapo muhimu ya kupanga mipango ya maendeleo kwa
wananchi kwa kuwafikishia huduma muhimu za kijamii katika maeneo yao kulingana
na mahitaji.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA), John Mkoma, alisema tayari anuani za makazi kwa nchi nzima
Zimekwisha kuandaliwa na kukamilika, hivyo hivi sasa jukumu lililopo ni
kuzisambaza pekee.
Mkoma alisema anuani hizo zilikwisha
kupitishwa na serikali na kutangazwa katika gazeti la serikali la Juni 22,
mwaka 2012, hivyo kuwa sheria.
Awali, akizungumza katika ufunguzi huo,
Mkurugenzi Mtendaji wa Universal Posta Union, Balozi Bisher Husein, alizitaka
serikali za nchi za Afrika kusaidia mashirika ya posta ya nchi zao kwa kuwa
yanafanya kazi kubwa kuwahudumia wananchi wa vipato vya chini.
CHANZO TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment