Arusha/Dar es Salaam. Wabunge wanne wa Chadema, ambao waliachiwa na
polisi kwa dhamana wamesimulia mateso waliyoyapata wakiwa rumande baada
ya kukamatwa juzi.
Vigogo hao; Mbunge wa Mpanda Mjini Said Amour Arfi, Tundu Lissu (Singida
Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti maalumu),
walikamatwa juzi baada ya wao na wafuasi wa chama hicho kutawanywa kwa
mabomu ya machozi na polisi kwenye Viwanja vya Soweto, Arusha.
Wabunge hao waliachiwa baada ya kujidhamini wenyewe huku watu wengine 65
waliokamatwa pamoja nao wakiachiwa baada ya kudhaminiwa.
Wote wanatakiwa kuripoti kwenye kituo hicho Julai 22, mwaka huu na wataelezwa hatma ya suala hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Operesheni wa Polisi,
Kamishna Paul Chagonja alisema jeshi lake linaendelea kuwasaka
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha,
Godbless Lema na kuwaonya kuwa wanatakiwa kujisalimisha mara moja.
Chagonja alisema Mbowe na Lema wanatafutwa kwa kosa la kufanya kusanyiko
lisilo halali katika viwanja hivyo vya Soweto walipokuwa wakitaka
kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi, Ramadhan Juma na Amir
Ally waliofariki dunia baada ya kuumizwa kutokana na mlipuko wa bomu,
Jumamosi iliyopita.
Pia aliwaamuru Mbowe na Lema kuwasilisha mara moja ushahidi wa
kuwahusisha polisi na shambulio la bomu na kama hawana imani na Polisi,
basi wawasilishe ushahidi wao kwa Rais Jakaya Kikwete.
Lissu
Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
alilalamikia kitendo cha polisi kumwagia maji ya kuwasha baada ya
kumkamata.
“Walinimwagia maji ya kuwasha kwa mfululizo nikalazimika kulala chini
kifudifudi huku nikiwa nimefunika macho kukwepa yasiingie maji. “Kuna
askari walitaka kunipiga lakini niliokolewa na mwenzao mmoja
aliyenikinga nisishambuliwe. Kwa kweli ilikuwa hali ya hatari,” alisema.
Alisema polisi hao waliomkamata walivunja miwani yake kwa makusudi akisema aliikabidhi kaunta ikiwa haijavunjika.
“Wakati naingia mahabusu nilikabidhi miwani yangu lakini ajabu wakati
tukiachiwa ilikuwa imevunjika.” Alilalamikia hatua ya polisi
kuwashambulia kwa mabomu, kuwamwagia maji ya kuwasha walipokuwa
wakiwatawanya watu waliokusanyika Soweto akisema awali, waliwaruhusu
“Kwa maoni yangu na maoni ya wenzangu, hakukuwa na sababu ya polisi
kupiga mabomu, risasi na kumwagia watu maji ya kuwasha kwani ni wao
ndiyo walituomba tubebe dhamana ya uongozi kwa kwenda kuwaomba wananchi
waliokusanyika pale uwanjani kutawanyika,” alisema Lissu.
Alisema Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Gilles Mroto ndiye
aliyewaruhusu kuzungumza na wananchi ili watawanyike baada ya viwanja
hivyo kuzuiwa kutumika kwa shughuli ya kuaga miili ya waliopoteza maisha
kwenye tukio la bomu.
Alisema pamoja na ruhusa hiyo, polisi waliwaruhusu Chadema kuchukua
magari yao yenye vipaza sauti ili wavitumie kuwatawanya wananchi hao
lakini ajabu polisi ikawapiga mabomu mara baada ya Arfi kuwataka
wananchi watawanyike kwenda Hospitali ya Mount Meru kutoa heshima za
mwisho kwa marehemu.
“Kama ule mkusanyiko haukuwa halali, kwa nini polisi haohao walikaa na
wananchi wale tangu asubuhi na wakaturuhusu kuzungumza nao ili
watawanyike?”
Alisema kisheria, mkusanyiko usio halali unastahili kusambaratishwa kwa
mabomu baada ya polisi kutoa ilani kwa wahusika kutawanyika tofauti na
juzi akisema hawakutoa ilani yoyote.
Akunaay
Akunaay alisema polisi wanapaswa kubadilisha mbinu za kukabiliana na
watu wanaodhani wamevunja sheria badala ya kukimbilia kupiga mabomu na
kufyatua risasi.
“Mabomu na risasi ni kukomaza watu na kuwafanya wazoee milipuko.
Itafikia hatua wananchi watajenga usugu na kuanza kupambana na polisi,”
alisema na kuongeza:
“Polisi baada ya kutukamata na kutuweka chini ya ulinzi walitupiga hadi
tukiwa kituoni bila sababu yoyote. Nadhani askari wetu wanapaswa kuacha
kumalizia hasira zao za magumu yao yanayowakabili kwa kuwapiga
watuhumiwa.”
Mukya
Mukya amelalamikia kitendo cha polisi kukataa kumpa fursa ya
kumnyonyesha mtoto wake mchanga akisema malaika huyo alilazimika
kushinda njaa kutwa nzima ya juzi na usiku kucha.
“Niliwaomba polisi wanikubalie kujidhamini au wanisindikize
nikamnyonyeshe mtoto lakini walinikatalia kama vile ninakabiliwa na kesi
ya mauaji,” alisema Mukya
Akizungumzia suala hilo, Mwenyeki wa Baraza la Wanawake wa Chadema
(Bawacha), Susan Lyimo alisema: “Ni kinyume cha taratibu za haki za
binadamu kwa mwanamke kunyimwa nafasi ya kunyonyesha mtoto wake.”
Polisi wajibu
Akizungumzia malalamiko ya wabunge hao, Kamishna Chagonja alisema hakuna
mtuhumiwa ambaye anaweza kutoka mahabusu akaimwagia sifa kwa sababu
siyo mahali pa kusifiwa, bali ni mahali penye kizuizi cha muda ili
kuwezesha mkondo wa sheria kuchukua nafasi yake.
“Hatuna (polisi), roho ya Adolph Hitler (dikteta wa zamani wa
Ujerumani), tupo kwa ajili ya kulinda wananchi na mali zao,” alisema.
Aidha, alikanusha madai ya Mukya ya kunyimwa ruhusa ya kumnyonyesha
mwanaye akisema: “Siku hizi kuna dawati la jinsia katika vituo vyetu vya
polisi kwa hiyo kama ni kunyonyesha lazima wangesimamia utaratibu wa
kumwezesha kufanya hivyo, siyo kweli kwamba amekataliwa, haya ni maneno
ya kulichafua jeshi.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema wanaojihusisha
na uhalifu wowote huwa na imani kuwa watafanikiwa kujificha au kukwepa
mkono wa dola na inapotokea wamekamatwa na kuchukuliwa hatua, huanza
kujitetea kwa kuwashushia lawama polisi.
“Hasa wanasiasa na wanaharakati wakikamatwa na kuwekwa rumande, wengi
hutoa manung’uniko mengi yakiwamo ya uongo, ilimradi kuchafua polisi
mbele ya wananchi. Hatupo kwa ajili ya kusifiwa, bali kutimiza wajibu
wetu,” alisema Sabas.
Kifo chaongezeka
Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mlipuko huo imefikia wanne
baada ya mtoto Fahad Jamal (7), aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya
Seliani kufariki dunia jana. Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Paul
Kisanga alithibitisha jana kufariki kwa majeruhi huyo aliyekuwa ameumia
kichwani na kulazwa kwenye chumba cha wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi
maalumu (ICU).
Mmoja kuagwa leo
Kiongozi wa Chadema, Judith Moshi aliyefariki kwenye tukio hilo la bomu,
leo anatarajiwa kuagwa kwa heshima zote za chama hicho katika moja ya
makanisa jijini Arusha baada ya polisi kukizuia chama hicho kuendesha
shughuli hiyo katika eneo la wazi.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema
baada ya kuagwa, marehemu Moshi atazikwa Arusha badala ya kusafirishwa
kwenda mkoani Kilimanjaro kama ilivyokuwa imepangwa awali ili kutoa
fursa kwa wananchi wa jiji hilo kushiriki katika mazishi yake
chanzo:mwananchi
0 comments:
Post a Comment