Arusha
Home » » WADAU WA KAHAWA WAZIOMBA HALMASHAURI KUWATENGEA MAFUNGU

WADAU WA KAHAWA WAZIOMBA HALMASHAURI KUWATENGEA MAFUNGU



IMG_4629
NA GLADNESS MUSHI, ARUSHA WADAU wa kahawa wameziomba halmashauri kutenga kiasi cha fedha katika mapato yao kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha kahawa kuliko kuendelea kudorora siku hadi siku kutokana na wakulima wengi kutoona faida yake.
Waliyasema hayo jana wakati wakizungumza katika mkutano uliwashirikisha wadau wa kahawa kutoka kanda ya kaskazini uliofanyika mjini hapa na kuandaliwa na bodi ya kahawa Tanzania, uliolenga kujadili jinsi ya kuboresha zao hilo na kujiandaa  kwa ajili ya mkutano mkuu wa wadau wa kahawa utakaofanyika may 30 hadi 31 mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkulima aliyejitambulisha kwa jina la Lemburis Sirikwa alisema kuwa , zao hilo limedorora sana kutokana na wakulima wengi waliokuwa wakilima zao hilo kubadilisha matumizi ya mashamba na kulima kilimo kingine kutokana na kutoona faida  yake.
Sirikwa alisema kuwa, biashara ya kahawa hapa nchini imeporomoka kwa asilimia 90 kutokana na kuwa wakulima wengi wa kahawa wamekuwa wakiishia kupata hasara siku hadi siku kutokana na zao hilo kutothaminiwa na serikali na kulichukulia uzito kama mazao mengine yalivyo.
” Lazima halmashauri zijikite katika kufufua zao hilo la kahawa katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutoa ruzuku za dawa za pembejeo ili kuwezesha wakulima hao kutotumia gharama nyingi katika uandaaji wa mashamba na mwishowe kuishia kupata hasara  kutokana na kutokuwa na masoko ya uhakika”alisema Sirikwa.
Naye Mkurugenzi wa maendeleo ya kahawa na uendeshaji bodi ya kahawa Tanzania , Godluck Sipira alisema kuwa, wameweza kukutana na wadau mbalimbali wa kahawa na kuweza kusikiliza changamoto zao ambapo  wameweza pia kutoka na maazimio ambayo watayawasilisha katika mkutano mkuu wa wadau wa kahawa na  kuyajadili na hatimaye kuyatolea utatuzi.
Sipira alisema kuwa,lengo ni kuhakikisha kuwa sekta nzima ya kahawa nchini inaendelezwa na kuweza kufufua zao la kahawa ambalo limeonekana kudorora katika maeneo mbalimbali hapa nchini kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima .
Aliongeza kuwa,ili zao hilo liweze kurudi kwenye hali yake ya kawaida ni wajibu wa kila mdau kujitahidi kutekeleza wajibu wake kwa nafasi yake katika kutumia rasilimali zilizopo katika kuhakikisha sekta ya kahawa inaimarika,na kusonga mbele katika kuleta tija ya kahawa. Naye mkuu wa wilaya ya Arumeru, Nyirembe Munasa aliitaka serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kahawa kuhakikisha kuwa wanaandaa utaratibu wa kuwapimia mashamba ya kahawa wakulima wa vijijini  ili kuweza kupata hati miliki na kuweza kupata mikopo katika mabenki na taasisi mbalimbali za kifedha.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa