Home » » WAJAWAZITO WATAKIWA KUHUDHURIA KLINIKI

WAJAWAZITO WATAKIWA KUHUDHURIA KLINIKI



Mary Mwita, Arumeru
WANAWAKE wajawazito wilayani Arusha, wametakiwa kujenga utamaduni wa kuhudhuria vituo vya afya ili waweze kujifungua salama na kuepuka vifo visivyo vya lazima.

Rai hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Selemani Rashid, wakati akizindua jengo la Zahanati ya Oldonyowasi iliyopo katika Kijiji cha Oldonyowasi, Kata ya Oldonyosambu.

Dk. Rashid alisema ni aibu wajawazito kujifungulia nyumbani, huku akiitaka jamii kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanawake kupenda kujitokeza na kuhudhuria kliniki, ili kupata ushauri wa daktari.

Aliwataka wananchi wa Kijiji cha Oldonyowasi kutumia Zahanati iliyojengwa kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo, ikiwamo msaada kutoka Ujerumani.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Arusha, Dk Thobias Mkina alisema kuwa Halmashauri hiyo inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa watumishi wa afya na kuiomba Serikali kupeleka watumishi zaidi.

Mkina alisema halmashauri hiyo imetoa vitanda kwa ajili ya Zahanati ya Odonyowasi na kueleza kuwa daktari kwa ajili ya zahanati hiyo atapelekwa kwa jili ya huduma.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sura Kijiji cha Oldonyowasi, Geofrey Ayo, aliwashukuru kwa msaada wa kujengewa zahanati hiyo na kufafanua kuwa hali ya huduma ya afya katika kijiji hicho ilikuwa mbaya kabla ya ujenzi wa zahanati hiyo.

Ayo alisema zahanati hiyo itasaidia kupunguza kama si kumaliza kabisa tatizo la vifo vya wajawazito na pia itachochea wananchi kujenga utamaduni wa kwenda hospitali badala ya kutumia miti shamba

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa