Na Nicodemus Ikonko,Hirondelle,Arusha
Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya
Rwanda (ICTR) Jumanne imempunguzia adhabu ya kifungo cha maisha jela hadi miaka
40,afisa mwandamizi wa zamani wa serikali ya Rwanda, Jean-Baptiste Gatete kwa
kuhusika kwake na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini mwake.
Mahakama imethibitisha kutiwa hatiani kwa Gatete kwa makosa ya mauaji ya
kimbari na kuteketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya binadamu. Mahakama ya awali
ilimpatia adhabu ya kifungo cha maisha jela, Machi 29, 2011 lakini Mahakama ya
Rufaa imempunguzia adhabu baada ya kukubali baadhi ya hoja zake za kukata
rufaa.Wakati wa mauaji ya kimbari Gatete alikuwa Mkurugenzi katika Wizara ya
Wanawake na Masuala ya Watoto.
‘’Mahakama ya Rufaa inabadili adhabu ya kifungo cha maisha jela alichopewa
Jean-Baptiste Gatete na kumpatia adhabu ya kifungo cha miaka 40 jela, ambayo
pia itazingatia muda aliokwishatumikia tangu atiwe kizuizini Septemba 11,
2002,’’ Jaji Kiongozi Liu Daqun alitamka.
Gatete aliyevaa mahakamani suti rangi ya maziwa alionekana akiwa
ametulia wakati hukumu hiyo ilipokuwa inasomwa mbele ya ukumbi wa mahakama
uliofurika wasikilizaji.
Kupunguziwa adhabu kutoka kifungo cha maisha hadi miaka 40 jela
kumetokana pia na mahakama ya awali kukiuka haki ya Gatete ya kusikilizwa kwa
kesi yake bila kucheleweshwa pasipo sababu za msingi. Alitiwa mbaroni Septemba
11, 2002 nchini Congo-Brazzaville lakini kesi yake ilianza kusikilizwa Oktoba
20,2009,ikiwa ni miaka saba baadaye.
Katika mahakama ya awali, Gatete ilionekana na hatia pasipo mashaka
yoyote kwa kuhusika na vifo vya mamia au hata maelfu ya Watutsi katika maeneo
matatu yalikofanyikia mauaji hayo, Mashariki mwa Rwanda kati ya Aprili 7 na 12,
1994.
Maeneo yalikotokea umwagaji damu mkubwa ni pamoja na yale ya kata ya
Rwankuba na parokia ya Kiziguro kwenye wilaya ya Murambi katika mkoa wa Byumba
na maeneo ya parokia ya Mukarange katika wilaya ya Kayonza, mkoa wa Kibungo.
Gatete (59) alitiwa mbaroni nchini Congo-Brazzaville Septemba 11, 2002
na kisha kuhamishiwa makao makuu ya ICTR, Arusha nchini Tanzania.
NI/FK
© Hirondelle News Agency
© Hirondelle News Agency
0 comments:
Post a Comment