Home » » SERIKALI KUPELEKA NISHATI MBADALA VIJIJINI

SERIKALI KUPELEKA NISHATI MBADALA VIJIJINI



Na Arodia Peter, Arusha
SERIKALI imesema imeanza kuelekeza nguvu kupeleka nishati ya umeme mbadala katika maeneo ya vijijini. Hayo yalibainishwa jana na Naibu wa Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, wakati akizindua mashindano ya kupeleka umeme huo vijijini.

Mashindano hayo yameandaliwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB).

Simbachawene alisema, Tanzania kuna vyanzo vingi vya kuwezesha upatikanaji wa umeme mbadala maeneo ya vijijini, ikiwemo upepo, jua na kinyesi cha wanyama (bio gas).

Washindi 15 kati ya 26 walioingia katika mashindano wanatarajiwa kupatikana, baada ya andiko lao la mradi kukidhi vigezo vilivyowekwa na REA.

Washindi hao ni wajasiriamali wa Kitanzania na watazawadiwa Sh milioni 150 kila mmoja, ambazo watazitumia kuendeleza miradi ya umeme vijijini.

Katika uzinduzi huo, Simbachawene alisema Tanzania imeamua kujikita katika sekta ya umeme mbadala kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa kushirikisha sekta binafsi.

Kwa mujibu wa naibu huyo, sera ya taifa ya mwaka 2003 inaelekeza umuhimu wa nishati katika maeneo ya vijijini.

Alisema kuendelea kutegemea umeme unaozalishwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), pekee ni kuchelewa kufikia haraka maendeleo ya wananchi.

“Nchi zilizoendelea zinategemea umeme mbadala kwa ajili ya kuendesha uchumi wao, Tanzania tuna kila sababu ya kuhakikisha nishati hiyo inawafikia watu wa vijijini.

“Ingawa miundombinu yote ya umeme iko chini ya TANESCO, kama wizara tumeamua kuelekeza nguvu kubwa huko, ili kila mwananchi aweze kupata mwanga na kuachana na matumizi ya vibatari, chemli na kuni, 

“Tunaamini miradi hii itasaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi maeneo ya vijijini, ili kutimiza malengo tuliyojiwekea katika sera yetu,” alisema Simbachawene.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Amy Mpungwe, alisema bodi yake imejipanga kuharakisha maagizo ya Serikali kuzifikia taasisi za kijamii zilizoko vijijini.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa