Na Eliya Mbonea, Arusha
RUFAA ya kupinga kuvuliwa ubunge wa aliyekuwa
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), inatarajiwa kusikilizwa kesho
na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, wakiongozwa na Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mohamed Chande.
Majaji wengine waliopo katika kusikiliza rufaa hiyo inayovuta hisia za watu
wengi ni pamoja na Jaji Natalia Kimaro na Salum Massati, wote wa Mahakama ya
Rufaa nchini.
Rufaa hiyo ambayo ilipaswa kusikilizwa Septemba 23, mwaka huu, ilisogezwa mbele
hadi Oktoba 2, kutokana na mawakili wa pande zote mbili kupatwa na dharura,
ambapo jopo hilo liliridhika na hivyo kusogeza mbele tarehe.
Jopo hilo lilizingatia barua iliyoomba kusogezwa mbele kwa shauri hilo hadi
Oktoba 2, kutokana na mawakili, Tundu Lissu, anayemtetea Lema na kaka yake,
Alute Mughwai, anayewatetea walalamikaji kufiwa na baba yao mzazi.
Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), anashirikiana
na Wakili Mwandamizi Method Kimomogoro katika kumtetea mrufani, Godbless Lema.
Kwa upande wake Wakili Mughwai anashirikiana na Wakili Modest Akida
kuwawakilisha wadaiwa katika shauri hilo ambao ni wanachama watatu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo.
Wanachama hao walifungua shauri lililotengua ubunge wa Lema wakidai kuwa wakati
wa kampeni alimdhalilisha aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Batilda Burian, kwa
kutumia lugha za matusi.
Awali, Lema kupitia wakili wake, Method Kimomogoro, anayesaidiana na Lissu,
aliwasilisha katika mahakama hiyo hoja 18 za madai, akipinga ubunge wake
kutenguliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu.
Katika baadhi ya madai hayo, Lema aliiomba Mahakama ya Rufaa kutengua uamuzi wa
Mahakama Kuu, huku akiitaka mahakama hiyo imtangaze kuwa mbunge halali wa Jimbo
la Arusha Mjini.
Aidha, aliitaka mahakama hiyo ya juu, iwaamuru walalamikiwa katika shauri hilo
walipe gharama za rufaa hiyo pamoja na gharama za kesi iliyomalizika katika
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Katika madai mengine, Lema anamlalamikia Jaji Gabriel Rwakibarila,
aliyesikiliza kesi hiyo kuwa alitoa uamuzi wake kwa kuzingatia maneno ya uvumi,
huku akipuuza ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment