Na Nicodemus Ikonko,
Hirondelle, Arusha
Mahakama ya Kimataifa ya
Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) imehitimisha majadiliano na Kamisheni ya
Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) ili kusimamia usikilizaji wa kesi za
mauaji ya kimbari zinazopelekwa kusikilizwa nchini Rwanda.
‘’Hali iliyopo sasa ni
kwamba ICTR kupitia ofisi ya Msajili imeshahitimisha majadiliano na ACHPR
kusimamia usikilizaji wa kesi,’’ Msemaji wa Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa,
Roland Amossouga aliliambia Shirika la Habari la Hirondelle Jumanne.
Aliongeza kwamba,’’Hati ya
makubaliano hayo itatiwa saini hivi karibuni na baada ya hapo ACHPR ndipo
itaanza rasmi kazi yake ya kusimamia kesi ya (Jean) Uwinkindi nchini Rwanda.’’
Wafanyakazi wawili wa ICTR waliteuliwa
Aprili mwaka huu kama wasimamizi wa muda wa kesi ya Uwinkindi, huku ACHPR
ikisubiriwa kukamilisha makubaliano na ICTR kufanya kazi hiyo. ACHPR ina
majukumu ya kulinda na kukuza haki za binadamu ikiwa ni miongoni mwa kazi
zake.
Wakati ukitolewa uamuzi wa
kuhamishia kesi ya Uwinkindi kwenda Rwanda Juni 2011, Majaji walimwelekeza
Msajili wa Mahakama ICTR kuingia katika mkataba wa maandishi na ACHPR ambao
utaeleza wazi maslahi, fedha zinazohitajika na mambo mengine muhimu ambayo
yatafanya taasisi hiyo kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Kwa mujibu wa majaji
‘’ACHPR itatakiwa kuwasilisha ripoti ya mara kwa mara kila baada ya miezi
mitatu juu ya hali ya mwenendo wa kesi kwa Rais wa ICTR kupitia kwa Msajili
wake, wakati kesi itakapoanza kusikilizwa hadi hapo itakapohitimishwa ikiwa ni
pamoja na hatua ya rufaa kwa mshitakiwa na pia katika hatua ya kusimamia adhabu
itakayotolewa, kama itakuwepo.’’
Majaji waliridhika kuwa
hatua ya Kamisheni hiyo kusimamia mwendendo mzima wa kesi utatoa hakikisho kwamba
ukiukwaji wowote wa haki ya mshitakiwa katika mwenendo wa kesi yake utapelekwa
mbele ya Rais wa ICTR mara moja ili hatua za kurekebisha zichukuliwe ikiwa ni
pamoja na kufikiria kuiondoa kesi hiyo kusikilizwa mbele ya mahakama za Rwanda.
ICTR tayari imeridhia kesi
nane kwenda kusikilizwa nchini Rwanda. Uwinkindi, ambaye ni mchungaji
alihamishiwa nchini Rwanda Aprili 19, 2012, akiwa ni mshitakiwa wa kwanza wa
ICTR kesi yake kwenda kusikilizwa nchini humo.
Nje ya Uwinkindi, kesi
nyingine zilizohamishiwa nchini Rwanda ni pomoja na mtuhumiwa ambaye bado
anashikiliwa na ICTR na kiongozi wa zamani wa wanamgambo wa Interahamwe,
watuhumiwa sita ambao bado wanasakwa, wakiwemo mameya watatu, polisi mmoja,
afisa wa zamani wa jeshi na meneja mmoja wa mgahawa. Hata hivyo kesi nyingine
mbili bado zipo mbele ya Mahakama ya Rufaa zikisubiri uamuzi.
NI/FK
© Hirondelle News Agency
0 comments:
Post a Comment