Na Nicodemus Ikonko, Hirondelle
Mwendesha
mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda
(ICTR),ameiomba mahakama hiyo kutupilia mbali maombi ya Waziri wa zamani
wa Habari wa Rwanda na mfungwa wa mauaji ya kimbari, Eliezer
Niyitegeka, anayetaka kufanyika kwa uchunguzi dhidi ya madai ya
mashahidi kutoa ushahidi wa uongo katika kesi yake.
‘’Niyitegeka
hajatoa kitu chochote kipya cha kuonyesha kuwepo kwa ushahidi wa uongo.
Juhudi zake za kujaribu kwa mara nyingine kupinga matokeo
yaliyobainishwa dhidi yake hapo awali hazina budi kutupiliwa mbali,’’
anaeleza James Arguin, Mkuu wa Kitengo cha Rufaa na Ushauri wa Kisheria,
katika ofisi ya Mwendesha Mashitaka anaeleza katika hati ya kujibu
maombi ya mfungwa huyo Jumatatu.
Waziri
huyo wa zamani ambaye hivi sasa anatumikia kifungo cha maisha jela
nchini Mali, alitiwa hatiani na mahakama ya awali Mei 23, 2003 kwa
tuhuma za mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu. Mahakama ya
Rufaa nayo ilithibitisha hukumu na adhabu aliyopewa Julai 9, 2004.
Mahakama
hiyo ya Umoja wa Mataifa imeshayakataa maombi matano kutoka kwa mfungwa
huyo yaliyotaka mahakama ifanye marejeo ya hukumu yake.
Katika
maombi yake, Niyitegeka anataka Mahakama imwamuru Msajili wa Mahakama
hiyo, imteue rafiki wa mahakama, kuchunguza ushahidi wa mashahidi wa
mwendesha mashitaka hususan ni shahidi mwenye jina bandia la GGV, kwa
lengo la kutaka hatimaye ashitakiwe kwa kutoa ushahidi wa uongo.
Kama
ombi hilo la awali halitakubalika mfungwa huyo anaomba afikiriwe ombi
lingine la kuondoa amri inayomlinda shahidi huyo kutotoa ushahidi wake
hadharani kwa kutumia jina bandia ili asitambulike kwa sababu za
kiusalama ili sasa atambulike hadharani na kisha ashitakiwe mbele ya
mahakama nyingine.
Maombi
ya Niyitegeka ya kuunda jopo la kusikiliza madai yake yalikubaliwa
Septemba 7, 2012 na tayari yamepangiwa jopo la majaji watatu
kuyasikiliza akiwemo Rais wa ICTR.
NI/FK
© Hirondelle News Agency
© Hirondelle News Agency
0 comments:
Post a Comment